‏ Revelation of John 5:8-14

8 aAlipokwisha kukitwaa kile kitabu, wale viumbe wenye uhai wanne pamoja na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele ya yule Mwana-Kondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi, nao walikuwa wameshika mabakuli ya dhahabu yaliyojaa uvumba, ambayo ni maombi ya watakatifu. 9 bNao wakaimba wimbo mpya, wakisema:

“Wewe unastahili kukitwaa kitabu
na kuzivunja lakiri zake,
kwa sababu ulichinjwa
na kwa damu yako ukamnunulia Mungu watu
kutoka kila kabila, kila lugha,
kila jamaa na kila taifa.
10 cWewe umewafanya hawa wawe ufalme na makuhani
wa kumtumikia Mungu wetu,
nao watatawala duniani.”
11 dKisha nikatazama, nikasikia sauti za malaika wengi wakiwa wamekizunguka kile kiti cha enzi, pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne. Idadi yao ilikuwa kumi elfu mara kumi elfu na maelfu ya maelfu. 12 eNao waliimba kwa sauti kuu, wakisema:

“Anastahili Mwana-Kondoo, yeye aliyechinjwa,
kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu
na heshima na utukufu na sifa!”
13 fKisha nikasikia kila kiumbe mbinguni na duniani, chini ya nchi na baharini na vyote vilivyomo ndani yake vikiimba:

“Sifa na heshima na utukufu na uweza
ni vyake yeye aketiye juu ya hicho kiti cha enzi
na kwa Mwana-Kondoo,
milele na milele!”
14 gWale viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amen!” Nao wale wazee ishirini na wanne wakaanguka kifudifudi wakaabudu.

Copyright information for SwhNEN