‏ Numbers 16:17-35

17 aKila mtu atachukua chetezo chake na kuweka uvumba ndani yake, vyetezo 250 kwa jumla, na kukileta mbele za Bwana. Wewe na Aroni mtaleta vyetezo vyenu pia.” 18Kwa hiyo kila mtu akachukua chetezo chake, akaweka moto na uvumba ndani yake, na kusimama pamoja na Mose na Aroni kwenye mlango wa Hema la Kukutania. 19 bKora alipokuwa amekusanya wafuasi wake wote kuwapinga Mose na Aroni kwenye mlango wa Hema la Kukutania, utukufu wa Bwana ukatokea kwa kusanyiko lote. 20Bwana akamwambia Mose na Aroni, 21 c“Jitengeni kutoka kwenye kusanyiko hili ili nipate kuwaangamiza mara moja.”

22 dLakini Mose na Aroni wakaanguka kufudifudi na kulia kwa sauti, wakasema, “Ee Mungu, Mungu wa roho za wanadamu wote, utakuwa na hasira na kusanyiko lote wakati ni mtu mmoja tu ametenda dhambi?”

23Ndipo Bwana akamwambia Mose, 24“Liambie kusanyiko, ‘Ondokeni hapo karibu na mahema ya Kora, Dathani na Abiramu.’ ”

25 eMose akainuka na kuwaendea Dathani na Abiramu, nao wazee wa Israeli wakafuatana naye. 26 fMose akalionya kusanyiko, “Sogeeni nyuma mbali na mahema ya hawa watu waovu! Msiguse kitu chochote kilicho mali yao, la sivyo mtafagiliwa mbali kwa sababu ya dhambi zao zote.” 27 gHivyo wakaondoka karibu na mahema ya Kora, Dathani na Abiramu. Dathani na Abiramu walikuwa wametoka nje, nao walikuwa wamesimama pamoja na wake zao, watoto wao na wale wanyonyao kwenye mlango wa mahema yao.

28 hNdipo Mose akasema, “Hivi ndivyo mtakavyojua kuwa Bwana amenituma kufanya mambo haya, na kwamba halikuwa wazo langu. 29 iIkiwa watu hawa watakufa kifo cha kawaida na kupatwa na yale ya kawaida yanayowapata wanadamu, basi Bwana hakunituma mimi. 30 jLakini ikiwa Bwana ataleta jambo jipya kabisa, ardhi ikifunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na kila kitu kilicho mali yao, nao washuke chini kaburini
Kaburini hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol.
wakiwa hai, ndipo mtafahamu kuwa watu hawa wamemdharau Bwana.”

31 lMara Mose alipomaliza kusema haya yote, ardhi iliyokuwa chini yao ikapasuka, 32 mnchi ikafunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na jamaa zao, na watu wote wa Kora na mali zao zote. 33 nWakashuka chini kaburini wakiwa hai, pamoja na kila kitu walichokuwa nacho; nchi ikajifunika juu yao, nao wakaangamia wakatoweka kutoka kusanyiko. 34Kutoka kilio chao, Waisraeli wote waliowazunguka walikimbia, wakipaza sauti, “Nchi inatumeza na sisi pia!”

35 oMoto ukaja kutoka kwa Bwana, ukawateketeza wale watu 250 waliokuwa wakifukiza uvumba.

Copyright information for SwhNEN