‏ Matthew 4:12-22

Yesu Aanza Kuhubiri

(Marko 1:14-15; Luka 4:14-15)

12 aYesu aliposikia kwamba Yohana Mbatizaji alikuwa ametiwa gerezani, alirudi Galilaya. 13 bAkaondoka Nazareti akaenda kuishi Kapernaumu, mji ulioko karibu na bahari, katika mipaka ya nchi ya Zabuloni na Naftali, 14 cili kutimiza unabii wa nabii Isaya, kama alivyosema:

15 d“Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali,
kwenye njia ya kuelekea baharini,
ngʼambo ya Yordani,
Galilaya ya watu wa Mataifa:
16 ewatu wale waliokaa gizani
wameona nuru kuu;
nao wale walioishi katika nchi ya uvuli wa mauti,
nuru imewazukia.”
17 fTangu wakati huo, Yesu alianza kuhubiri akisema: “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia.”

Yesu Awaita Wanafunzi Wake Wa Kwanza

(Marko 1:16-20; Luka 5:1-11)

18 gYesu alipokuwa anatembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea ndugu yake. Walikuwa wakizitupa nyavu zao baharini kwa kuwa wao walikuwa wavuvi. 19 hYesu akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.” 20 iMara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.

21 jAlipoendelea mbele kutoka pale, akawaona ndugu wengine wawili, Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa wamekaa kwenye mashua pamoja na baba yao Zebedayo, wakizitengeneza nyavu zao. Yesu akawaita. 22 kNao mara wakaiacha mashua yao, pamoja na baba yao, wakamfuata.

Copyright information for SwhNEN