Matthew 26:47-56
Yesu Akamatwa
(Marko 14:43-50; Luka 22:47-53; Yohana 18:3-12)
47 aAlipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale Kumi na Wawili, akafika. Alikuwa amefuatana na umati mkubwa wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 48Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni.” 49 bMara Yuda akamjia Yesu na kumsalimu, “Salamu, Rabi!” Akambusu.50 cYesu akamwambia, “Rafiki, fanya kile ulichokuja kufanya hapa.”
Kisha wale watu wakasogea mbele, wakamkamata Yesu. 51 dGhafula mmoja wa wale waliokuwa na Yesu alipoona hivyo, akaushika upanga wake, akauchomoa na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.
52 eNdipo Yesu akamwambia, “Rudisha upanga wako mahali pake, kwa maana wote watumiao upanga watakufa kwa upanga. 53 fJe, unadhani siwezi kumwomba Baba yangu naye mara moja akaniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? 54 gLakini je, yale Maandiko yanayotabiri kwamba ni lazima itendeke hivi yatatimiaje?”
55 hWakati huo, Yesu akawaambia ule umati wa watu, “Je, mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi? Siku kwa siku niliketi Hekaluni nikifundisha, mbona hamkunikamata? 56 iLakini haya yote yametukia ili maandiko ya manabii yapate kutimia.” Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha na kukimbia.
Copyright information for
SwhNEN