Mark 8:31-38
Yesu Atabiri Kifo Chake
(Mathayo 16:21-28; Luka 9:22-27)
31 aNdipo akaanza kuwafundisha wanafunzi wake kuwa Mwana wa Adamu lazima atapata mateso mengi na kukataliwa na wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa sheria, na kwamba itampasa auawe lakini baada ya siku tatu afufuke. 32 bAliyasema haya waziwazi, ndipo Petro akamchukua kando na akaanza kumkemea.33 cLakini Yesu alipogeuka na kuwaangalia wanafunzi wake, akamkemea Petro. Akasema, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”
34 dNdipo akauita ule umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, akasema, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. 35 eKwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili atayaokoa. 36Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? 37Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? 38 fMtu yeyote akinionea aibu mimi na maneno yangu katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu naye atamwonea aibu wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.”
Mark 9:1
1 gYesu akaendelea kuwaambia, “Amin, nawaambia, kuna watu waliosimama hapa ambao hawataonja mauti kabla ya kuuona Ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu.”
Copyright information for
SwhNEN