‏ Malachi 2:10-16

Yuda Si Mwaminifu

10 aJe, sote hatuna Baba mmoja? Hatukuumbwa na Mungu mmoja? Kwa nini basi tunalinajisi Agano la baba zetu kwa kukosa uaminifu kila mmoja kwa mwenzake?

11 bYuda amevunja uaminifu. Jambo la kuchukiza limetendeka katika Israeli na katika Yerusalemu: Yuda amepanajisi mahali patakatifu apendapo Bwana, kwa kuoa binti wa mungu mgeni. 12Kwa maana kwa mtu yeyote atendaye jambo hili, Bwana na amkatilie mbali kutoka hema za Yakobo, hata kama huwa anamletea Bwana Mwenye Nguvu Zote sadaka.

13 cKitu kingine mnachokifanya: Mnaifurikisha madhabahu ya Bwana kwa machozi. Mnalia na kuugua kwa sababu yeye haziangalii tena sadaka zenu wala hazikubali kwa furaha kutoka mikononi mwenu. 14 dMnauliza, “Kwa nini?” Ni kwa sababu Bwana ni shahidi kati yako na mke wa ujana wako, kwa sababu umevunja uaminifu naye, ingawa yeye ni mwenzako, mke wa agano lako la ndoa.

15 eJe, Bwana hakuwafanya wao kuwa mmoja? Katika mwili na katika roho wao ni wa Mungu. Kwa nini wawe mmoja? Kwa sababu Mungu alikuwa akitafuta mzao mwenye kumcha Mungu. Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, mtu asivunje uaminifu kwa mke wa ujana wake.

16 f“Ninachukia kuachana,” asema Bwana, Mungu wa Israeli, “pia nachukia mtu anayejivika jeuri kama vazi,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.

Kwa hiyo jihadharini wenyewe katika roho zenu, wala msije mkavunja uaminifu.

Copyright information for SwhNEN