‏ Luke 23:13-25

Yesu Ahukumiwa Kifo

(Mathayo 27:15-26; Marko 15:6-15; Yohana 18:39–19:16)

13 aBasi Pilato akawaita pamoja viongozi wa makuhani, viongozi wengine na watu, 14 bakawaambia, “Ninyi mlimleta huyu mtu kwangu kana kwamba ni mtu anayewachochea watu ili waasi. Nimemhoji mbele yenu nami nimeona hakuna msingi wowote wa mashtaka yenu dhidi yake. 15Wala Herode hakumwona na kosa lolote, ndiyo sababu amemrudisha kwetu. Kama mnavyoona, mtu huyu hakufanya jambo lolote linalostahili kifo. 16 cKwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi na kumwachia.” [ 17 dKwa kuwa ilikuwa lazima kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa Sikukuu.]

18 eNdipo watu wote wakapiga kelele kwa pamoja, “Mwondoe mtu huyo! Tufungulie Baraba!” 19(Baraba alikuwa amefungwa gerezani kwa sababu ya maasi yaliyokuwa yametokea mjini, na kwa ajili ya uuaji.)

20Pilato, akitaka kumwachia Yesu, akasema nao tena. 21Lakini wao wakaendelea kupiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!”

22 fKwa mara ya tatu, Pilato akawauliza, “Kwani amefanya kosa gani huyu mtu? Sikuona kwake sababu yoyote inayostahili adhabu ya kifo. Kwa hiyo nitaamuru apigwe mijeledi, na kisha nitamwachia.”

23Lakini watu wakazidi kupiga kelele kwa nguvu zaidi, wakidai kwamba Yesu asulubiwe. Hivyo, kelele zao zikashinda. 24 gKwa hiyo Pilato akatoa hukumu kwamba madai yao yatimizwe. 25Akamfungua yule mtu aliyekuwa amefungwa gerezani kwa kuhusika katika uasi dhidi ya serikali na mauaji. Akamkabidhi Yesu mikononi mwao, wamfanyie watakavyo.

Copyright information for SwhNEN