‏ Luke 22:7-23

Maandalizi Ya Pasaka

(Mathayo 26:17-25; Marko 14:12-21; Yohana 13:21-30)

7 aBasi ikawadia siku ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa. 8 bHivyo Yesu akawatuma Petro na Yohana, akisema, “Nendeni mkatuandalie chakula cha Pasaka ili tuweze kuila.”

9Wakamuuliza, “Unataka tukuandalie wapi?”

10Yesu akawaambia, “Tazameni, mtakapokuwa mkiingia mjini, mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka kwenye nyumba atakayoingia. 11Nanyi mwambieni mwenye nyumba, ‘Mwalimu anauliza: Kiko wapi chumba cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’ 12Atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani, kikiwa kimepambwa vizuri. Andaeni humo.”

13 cWakaenda, nao wakakuta kila kitu kama Yesu alivyowaambia. Hivyo wakaiandaa Pasaka.

Kuanzishwa Kwa Meza Ya Bwana

(Mathayo 26:31-35; Marko 14:27-31; Yohana 13:36-38)

14 dWakati ulipowadia, Yesu akaketi mezani pamoja na wale mitume wake. 15 eKisha akawaambia, “Nimetamani sana kuila Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu. 16 fKwa maana, nawaambia, sitaila tena Pasaka mpaka itakapotimizwa katika Ufalme wa Mungu.”

17Akiisha kukichukua kikombe, akashukuru, akasema, “Chukueni hiki mnywe wote. 18 gKwa maana nawaambia tangu sasa sitakunywa tena katika uzao wa mzabibu, hadi Ufalme wa Mungu utakapokuja.”

19 hKisha akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa, akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”

20 iVivyo hivyo baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, imwagikayo kwa ajili yenu. 21 jLakini mkono wake huyo atakayenisaliti uko hapa mezani pamoja nami. 22 kMwana wa Adamu anaenda zake kama ilivyokusudiwa. Lakini ole wake mtu huyo amsalitiye.” 23 lWakaanza kuulizana wenyewe ni nani miongoni mwao angeweza kufanya jambo hilo.

Copyright information for SwhNEN