‏ Luke 20:9-19

Mfano Wa Wapangaji Waovu

(Mathayo 21:33-46; Marko 12:1-12)

9 aAkaendelea kuwaambia watu mfano huu: “Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akalikodisha kwa wakulima fulani, kisha akasafiri kwa muda mrefu. 10 bWakati wa mavuno ulipofika, akamtuma mtumishi wake kwa hao wapangaji ili wampe sehemu ya mavuno ya shamba la mizabibu. Lakini wale wakulima wakampiga, wakamfukuza mikono mitupu. 11Akamtuma mtumishi mwingine, huyo naye wakampiga, wakamfanyia mambo ya aibu na kumfukuza. 12Bado akamtuma na mwingine wa tatu, huyu pia wakamjeruhi na kumtupa nje ya shamba.

13 c “Basi yule mwenye shamba la mizabibu akasema, ‘Nifanye nini? Nitamtuma mwanangu mpendwa, huenda yeye watamheshimu.’

14 “Lakini wale wapangaji walipomwona, wakasemezana wao kwa wao. Wakasema, ‘Huyu ndiye mrithi. Basi na tumuue ili urithi uwe wetu.’ 15Kwa hiyo wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamuua.”

“Sasa basi yule mwenye shamba la mizabibu atawafanyia nini wapangaji hawa?
16 dAtakuja na kuwaua hao wapangaji, na kuwapa wapangaji wengine hilo shamba la mizabibu.”

Watu waliposikia hayo wakasema, “Mungu apishie mbali jambo hili lisitokee!”

17 eLakini Yesu akawakazia macho, akasema, “Basi ni nini maana ya yale yaliyoandikwa:

“ ‘Jiwe walilolikataa waashi,
limekuwa jiwe kuu la pembeni’?
18 f Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagwa kabisa.”

19 gWalimu wa sheria na viongozi wa makuhani wakatafuta njia ya kumkamata mara moja, kwa sababu walifahamu kwamba amesema mfano huo kwa ajili yao. Lakini waliwaogopa watu.

Copyright information for SwhNEN