‏ Joshua 20

Miji Ya Makimbilio

(Hesabu 35:9-34)

1Ndipo Bwana akamwambia Yoshua, 2 a“Waambie Waisraeli, watenge miji mikubwa ya kukimbilia, kama nilivyokuagiza kupitia Mose, 3 bili mtu yeyote atakayemuua mtu kwa bahati mbaya na pasipo kukusudia aweze kukimbilia huko na kujiepusha na mlipiza kisasi wa damu.

4 c“Anapokimbilia mojawapo ya hii miji mikubwa atasimama kwenye maingilio ya lango la mji mkuu na kueleza wazee wa mji kuhusu shauri lake. Kisha watampokea katika mji wao na kumpa mahali pa kuishi nao. 5 dKama mlipiza kisasi wa damu akimfuatilia, wasimkabidhi yule mshtakiwa, kwa sababu alimuua jirani yake bila kukusudia, na bila kuwa na nia ya kudhuru. 6 eHuyu aliyeua atakaa kwenye mji mkubwa huo mpaka awe amesimama kukabili mashtaka yake mbele ya kusanyiko na mpaka kuhani mkuu anayehudumu kwa wakati huo atakapokufa. Ndipo atakapoweza kurudi nyumbani kwake katika mji ambao aliukimbia.”

7 fBasi wakatenga Kedeshi katika Galilaya kwenye nchi ya vilima ya Naftali, Shekemu katika nchi ya vilima ya Efraimu, na Kiriath-Arba (yaani Hebroni) kwenye nchi ya vilima ya Yuda. 8 gKatika upande wa mashariki mwa Yordani ya Yeriko wakatenga Bezeri katika jangwa katika uwanda wa juu katika kabila la Reubeni, Ramothi katika Gileadi katika kabila la Gadi, na Golani huko Bashani katika kabila la Manase. 9 hMwisraeli yeyote au mgeni yeyote aishiye miongoni mwao aliyemuua mtu kwa bahati mbaya, angeweza kukimbilia katika miji mikubwa hiyo iliyotengwa na asiuawe na mlipiza kisasi wa damu kabla hajasimama kukabili mashtaka mbele ya kusanyiko.

Copyright information for SwhNEN