John 20:3-19
3 aPetro na yule mwanafunzi mwingine wakaondoka mara kuelekea kaburini. 4Wote wawili walikuwa wanakimbia, lakini yule mwanafunzi mwingine akakimbia mbio zaidi kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini. 5 bAlipofika, akainama na kuchungulia mle kaburini, akaona vile vitambaa vya kitani mle ndani, lakini hakuingia. 6Ndipo Simoni Petro akaja, akimfuata nyuma akaenda moja kwa moja hadi ndani ya kaburi. Naye akaona vile vitambaa vya ile sanda vikiwa pale chini 7 cna kile kitambaa kilichokuwa kichwani mwa Yesu. Kitambaa hicho kilikuwa kimekunjwa mahali pa peke yake, mbali na vile vitambaa vya kitani vya ile sanda. 8 dKisha yule mwanafunzi aliyetangulia kufika kaburini naye akaingia ndani, akaona, akaamini, 9 e(kwa kuwa mpaka wakati huo walikuwa bado hawajaelewa kutoka Maandiko kwamba ilikuwa lazima Yesu afufuke kutoka kwa wafu).10Kisha hao wanafunzi wakaondoka wakarudi nyumbani kwao.
Yesu Anamtokea Maria Magdalene
(Mathayo 28:9-10; Marko 16:9-11)
11 fLakini Maria Magdalene akasimama nje ya kaburi akilia. Alipokuwa akilia, akainama, kuchungulia mle kaburini, 12 gnaye akaona malaika wawili wamevaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Yesu ulipokuwa umelazwa, mmoja upande wa kichwani na mwingine upande wa miguuni.13 hWakamuuliza Maria, “Mwanamke, mbona unalia?”
Akawaambia, “Nalia kwa kuwa wamemchukua Bwana wangu na sijui walikomweka.” 14 iBaada ya kusema hayo, akageuka, akamwona Yesu amesimama, lakini hakumtambua.
15 jYesu akamwambia, “Mwanamke, mbona unalia? Unamtafuta nani?”
Maria akidhani ya kuwa aliyekuwa anaongea naye ni mtunza bustani, kwa hiyo akamwambia, “Bwana, kama ni wewe umemchukua, tafadhali nionyeshe ulikomweka, nami nitamchukua.”
16 kYesu akamwita, “Maria!”
Ndipo Maria akamgeukia Yesu na kusema naye kwa Kiebrania, “Rabboni!” (maana yake Mwalimu).
17 lYesu akamwambia, “Usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ‘Ninapaa kwenda kwa Baba yangu ambaye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu ambaye ni Mungu wenu.’ ”
18 mKwa hiyo Maria Magdalene akaenda kuwatangazia wanafunzi wa Yesu, akisema, “Nimemwona Bwana!” Naye akawaambia kwamba Yesu alikuwa amemweleza mambo hayo yote.
Yesu Awatokea Wanafunzi Wake
(Mathayo 28:16-20; Marko 16:14-18; Luka 24:36-49)
19Ikawa jioni ya ile siku ya kwanza ya juma, wanafunzi wake walikuwa pamoja, milango ikiwa imefungwa kwa kuwaogopa Wayahudi. Naye Yesu aliwatokea, akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!”
Copyright information for
SwhNEN