‏ Jeremiah 42:9-22

9Akawaambia, “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye mlinituma kuwasilisha maombi yenu: 10 a‘Kama mkikaa katika nchi hii, nitawajenga wala sitawabomoa, nitawapanda wala sitawangʼoa, kwani ninahuzunishwa na maafa niliyowapiga nayo. 11 bMsimwogope mfalme wa Babeli, ambaye sasa mnamwogopa. Msimwogope, asema Bwana, kwa kuwa niko pamoja nanyi, nami nitawaokoa na kuwaponya kutoka mikononi mwake. 12 cNitawaonea huruma ili naye awe na huruma nanyi na kuwarudisha katika nchi yenu.’

13 d“Hata hivyo, kama mkisema, ‘Hatutakaa katika nchi hii,’ hivyo mkaacha kumtii Bwana Mungu wenu, 14 enanyi kama mkisema, ‘Hapana, tutakwenda kuishi Misri, mahali ambapo hatutaona vita au kusikia sauti ya tarumbeta au kuwa na njaa ya chakula,’ 15basi sikieni neno la Bwana, enyi mabaki ya Yuda. Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Ikiwa mmekusudia kwenda Misri na kufanya makazi huko, 16 fbasi ule upanga mnaouogopa utawapata huko, na njaa mnayoihofia itawafuata huko Misri, nanyi mtafia huko. 17 gNaam, wote waliokusudia kwenda kuishi Misri watakufa kwa upanga, njaa na tauni; hakuna hata mmoja wao atakayenusurika au kuokoka maafa nitakayoyaleta juu yao.’ 18 hHili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Kama vile hasira yangu na ghadhabu yangu ilivyomwagwa juu ya wale walioishi Yerusalemu, ndivyo ghadhabu yangu itakavyomwagwa juu yenu mtakapokwenda Misri. Mtakuwa kitu cha kulaania na cha kutisha, cha kulaumia na cha kushutumia, nanyi kamwe hamtaona mahali hapa tena.’

19 i“Enyi mabaki ya Yuda, Bwana amewaambia, ‘Msiende Misri.’ Hakikisheni jambo hili: Ninawaonya leo 20 jkwamba mmefanya kosa kubwa mioyoni mwenu mliponituma kwa Bwana Mungu wenu na kusema, ‘Mwombe Bwana Mungu wetu kwa ajili yetu, nawe utuambie kila kitu atakachosema, nasi tutafanya.’ 21 kNimewaambieni leo, lakini bado ninyi hamtaki kumtii Bwana Mungu wenu katika yote aliyonituma niwaambie. 22 lBasi sasa, hakikisheni jambo hili: Mtakufa kwa upanga, njaa na tauni mahali ambapo mnataka kwenda kuishi.”

Copyright information for SwhNEN