‏ Jeremiah 3:1-12

Israeli Asiye Mwaminifu

1 a“Kama mtu akimpa talaka mkewe,
naye akamwacha na akaolewa na mtu mwingine,
je, huyo mume aweza kumrudia tena?
Je, hiyo nchi haitanajisika kabisa?
Lakini umeishi kama kahaba na wapenzi wengi:
je, sasa utanirudia tena?”
asema Bwana.
2 b“Inua macho utazame miinuko iliyo kame na uone.
Je, pana mahali ambapo hawajalala nawe?
Uliketi kando ya barabara ukiwasubiri wapenzi,
ukakaa kama yeye ahamahamaye jangwani.
Umeinajisi nchi
kwa ukahaba wako na uovu wako.
3 cKwa hiyo mvua imezuiliwa,
nazo mvua za vuli hazikunyesha.
Hata hivyo, una uso usio na haya kama wa kahaba;
unakataa kutahayari kwa aibu.
4 dJe, wewe hujaniita hivi punde tu:
‘Baba yangu, rafiki yangu tangu ujana wangu,
5 eje, utakasirika siku zote?
Je, ghadhabu yako itaendelea milele?’
Hivi ndivyo unavyozungumza,
lakini unafanya maovu yote uwezayo.”

Wito Kwa Ajili Ya Toba

6 fWakati wa utawala wa Mfalme Yosia, Bwana aliniambia, “Umeona kile Israeli asiye mwaminifu amekifanya? Amepanda juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti uliotanda na amefanya uzinzi huko. 7 gMimi nilifikiri kuwa baada ya kuyafanya yote haya angelinirudia, lakini hakurudi, naye dada yake Yuda mdanganyifu aliona hili. 8 hNilimpa Israeli asiye mwaminifu hati yake ya talaka, na kumfukuza kwa ajili ya uzinzi wake wote. Hata hivyo nikaona kuwa Yuda dada yake mdanganyifu hakuogopa. Yeye pia alitoka na kufanya uzinzi. 9 iKwa sababu uasherati wa Israeli haukuwa kitu kwake, Yuda aliinajisi nchi kwa kuzini na mawe na miti. 10 jPamoja na hayo yote, Yuda dada yake mdanganyifu hakunirudia kwa moyo wake wote, bali kwa kujifanya tu,” asema Bwana.

11 k Bwana akaniambia, “Israeli asiye mwaminifu ana haki kuliko Yuda mdanganyifu. 12 lNenda, ukatangaze ujumbe huu kuelekea kaskazini:

“ ‘Rudi, Israeli usiye mwaminifu,’ asema Bwana,
‘sitakutazama tena kwa uso uliokunjamana,
kwa kuwa mimi ni mwenye huruma,’ asema Bwana,
‘Sitashika hasira yangu milele.
Copyright information for SwhNEN