Isaiah 37:1-20
Kuokolewa Kwa Yerusalemu Kunatabiriwa
(2 Wafalme 19:1-7)
1 aMfalme Hezekia aliposikia haya, akararua nguo zake na kuvaa nguo ya gunia, naye akaenda katika Hekalu la Bwana. 2 bAkawatuma Eliakimu msimamizi wa nyumba ya mfalme, Shebna mwandishi, na viongozi wa makuhani, wote wakiwa wamevaa nguo za magunia, waende kwa nabii Isaya mwana wa Amozi. 3 cWakamwambia, “Hili ndilo asemalo Hezekia: Siku hii ni siku ya dhiki, ya kukaripiwa na ya aibu, kama wakati watoto wanapofikia karibu kuzaliwa na kumbe hakuna nguvu ya kuwazaa. 4 dYamkini Bwana, Mungu wako atayasikia maneno ya jemadari wa jeshi, ambaye bwana wake, mfalme wa Ashuru, amemtuma kumdhihaki Mungu aliye hai, tena kwamba atamkemea kwa maneno ambayo Bwana, Mungu wako ameyasikia. Kwa hiyo omba kwa ajili ya mabaki ambao bado wako.”5Maafisa wa Mfalme Hezekia walipofika kwa Isaya, 6 eIsaya akawaambia, “Mwambieni bwana wenu, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Usiogope kwa hayo uliyoyasikia, yale maneno ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana nayo. 7 fSikiliza! Nitatia roho fulani ndani yake ili kwamba atakaposikia taarifa fulani, atarudi nchi yake mwenyewe, nami huko nitafanya auawe kwa upanga.’ ”
8 gJemadari wa jeshi aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru ameondoka Lakishi, alirudi, akamkuta mfalme akipigana na Libna.
9 hBasi Senakeribu akapata taarifa kwamba Tirhaka, Mkushi mfalme wa Misri, alikuwa anaenda kupigana naye. Aliposikia jambo hili akatuma wajumbe kwa Hezekia na neno hili: 10 i“Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda: Usikubali huyo Mungu unayemtumainia akudanganye wakati anaposema, ‘Yerusalemu haitatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.’ 11 jHakika umesikia yale ambayo wafalme wa Ashuru wametenda kwa nchi zote, wakiwaangamiza kabisa. Je, wewe utaokolewa? 12 kJe, miungu ya mataifa ambayo yaliangamizwa na baba zangu iliweza kuwaokoa? Yaani miungu ya Gozani, Harani, Resefu, na ya watu wa Edeni waliokuwa Telasari? 13 lYuko wapi mfalme wa Hamathi, mfalme wa Arpadi, mfalme wa mji wa Sefarvaimu, au wa Hena au wa Iva?”
Maombi Ya Hezekia
14 mHezekia akapokea barua kutoka kwa wale wajumbe naye akaisoma. Kisha akapanda katika Hekalu la Bwana, akaikunjua mbele za Bwana. 15 nNaye Hezekia akamwomba Bwana akisema: 16 o“Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, uketiye juu ya kiti cha enzi kati ya makerubi, wewe peke yako ndiwe Mungu juu ya falme zote za dunia. Wewe umeumba mbingu na nchi. 17 pTega sikio, Ee Bwana, usikie; fungua macho yako, Ee Bwana, uone; sikiliza maneno yote ambayo Senakeribu ametuma kumtukana Mungu aliye hai.18 q“Ni kweli, Ee Bwana, kwamba wafalme wa Ashuru wameyaangamiza mataifa haya yote pamoja na nchi zao. 19 rWameitupa miungu yao kwenye moto na kuiangamiza, kwa kuwa haikuwa miungu, bali miti na mawe tu, iliyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. 20 sSasa basi, Ee Bwana Mungu wetu, tuokoe kutoka mkononi mwake, ili kwamba falme zote duniani zipate kujua kwamba wewe peke yako, Ee Bwana, ndiwe Mungu.”
Copyright information for
SwhNEN