Genesis 48:8-22
8 aWakati Israeli alipowaona wana wa Yosefu, akauliza, “Hawa ni nani?”9 bYosefu akamjibu baba yake, “Hawa ni wana ambao Mungu amenipa nikiwa huku.”
Ndipo Israeli akasema, “Walete kwangu ili niwabariki.”
10 cBasi macho ya Israeli yalikuwa hayaoni vizuri kwa sababu ya uzee, naye aliona kwa shida. Kwa hiyo Yosefu akawaleta wanawe karibu na baba yake, Israeli akawabusu na akawakumbatia.
11 dIsraeli akamwambia Yosefu, “Kamwe sikutazamia kuuona uso wako tena, lakini sasa Mungu ameniruhusu kuwaona watoto wako pia.”
12Ndipo Yosefu akawaondoa wanawe magotini mwa Israeli naye akasujudu hadi nchi. 13 eYosefu akachukua wale wana wawili, Efraimu kwenye mkono wake wa kuume akimwelekeza kwenye mkono wa kushoto wa Israeli, na Manase katika mkono wake wa kushoto akimwelekeza kwenye mkono wa kuume wa Israeli, akawaleta karibu na babu yao. 14Lakini Israeli akaupeleka mkono wake wa kuume, akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, ingawa alikuwa ndiye mdogo, na mkono wake wa kushoto akaukatisha, akauweka juu ya kichwa cha Manase, ingawa Manase alikuwa ndiye mzaliwa wa kwanza.
15Ndipo akambariki Yosefu akisema,
“Mungu ambaye baba zangu
Abrahamu na Isaki walimtii,
Mungu ambaye amekuwa mchungaji
wa maisha yangu yote mpaka leo hii,
16 fMalaika ambaye aliniokoa kutoka madhara yote,
yeye na awabariki vijana hawa.
Na waitwe kwa jina langu
na kwa majina ya baba zangu Abrahamu na Isaki,
wao na waongezeke kwa wingi
katika dunia.”
17 gYosefu alipoona baba yake akiweka mkono wa kuume juu ya kichwa cha Efraimu, hakupendezwa, kwa hiyo akauchukua mkono wa baba yake kutoka kichwa cha Efraimu na kuuweka juu ya kichwa cha Manase. 18 hYosefu akamwambia, “Hapana, baba yangu, huyu ndiye mzaliwa wa kwanza; uweke mkono wako wa kuume juu ya kichwa chake.”
19 iLakini baba yake akakataa, akasema, “Ninajua, mwanangu, ninajua. Yeye pia atakuwa taifa, naye pia atakuwa mkuu. Hata hivyo, ndugu yake mdogo atakuwa mkuu kuliko yeye, nao wazao wake watakuwa kundi la mataifa.” 20 jAkawabarikia siku ile na kusema,
“Kwa jina lenu Israeli watatamka baraka hii:
‘Mungu na awafanye kama Efraimu na Manase.’ ”
Kwa hiyo akamtanguliza Efraimu mbele ya Manase.
21 kNdipo Israeli akamwambia Yosefu, “Mimi ninakaribia kufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, na atawarudisha katika nchi ya baba zenu. 22 lKwako wewe, kama aliye juu ya ndugu zako, ninakupa sehemu moja zaidi ya ndugu zako, lile eneo nililoteka kwa Waamori kwa upanga wangu na upinde wangu.”
Copyright information for
SwhNEN