‏ Genesis 22:2-13

2 aKisha Mungu akamwambia, “Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, Isaki umpendaye, uende katika nchi ya Moria. Mtoe huko kama sadaka ya kuteketezwa juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.”

3 bAbrahamu akaamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, akamtayarisha punda wake. Akawachukua watumishi wake wawili pamoja na Isaki mwanawe. Baada ya kuchanja kuni za kutosha kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka kuelekea mahali Mungu alipokuwa amemwambia. 4Siku ya tatu Abrahamu akainua macho, akapaona mahali pale kwa mbali. 5 cAkawaambia watumishi wake, “Kaeni hapa pamoja na punda, wakati mimi na kijana tunakwenda kule. Tutakwenda kuabudu na kisha tutawarudia.”

6 dAbrahamu akachukua kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, akamtwika Isaki mwanawe, yeye mwenyewe akachukua moto na kisu. Walipokuwa wakienda pamoja, 7 eIsaki akanena akamwambia Abrahamu baba yake, “Baba yangu!”

Abrahamu akaitika, “Mimi hapa, mwanangu.”

Isaki akasema, “Moto na kuni zipo, Je, yuko wapi mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa?”

8 fAbrahamu akajibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atajipatia mwana-kondoo kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa.” Nao hawa wawili wakaendelea mbele pamoja.

9 gWalipofika mahali pale alipokuwa ameambiwa na Mungu, Abrahamu akajenga madhabahu hapo, akaziweka kuni juu yake. Akamfunga Isaki mwanawe na akamlaza kwenye madhabahu, juu ya zile kuni. 10 hKisha akanyoosha mkono wake na akachukua kisu ili amchinje mwanawe. 11 iLakini malaika wa Bwana akamwita kutoka mbinguni, akamwambia, “Abrahamu! Abrahamu!”

Akajibu, “Mimi hapa.”

12 jAkamwambia, “Usimdhuru kijana, wala usimtendee jambo lolote. Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwa sababu hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee.”

13 kAbrahamu akainua macho yake, akaona kondoo dume amenaswa pembe zake nyuma yake katika kichaka. Akaenda akamchukua huyo kondoo dume, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.
Copyright information for SwhNEN