Ezekiel 11:1-22
Hukumu Juu Ya Viongozi Wa Israeli
1 aNdipo Roho akaniinua na kunileta mpaka kwenye lango la nyumba ya Bwana linalotazama upande wa mashariki. Pale kwenye ingilio la lango kulikuwepo wanaume ishirini na watano, nami nikaona miongoni mwao Yaazania mwana wa Azuri na Pelatia mwana wa Benaya, viongozi wa watu. 2 bBwana akaniambia, “Mwanadamu, hawa ndio wafanyao hila na kutoa mashauri potovu katika mji huu. 3 cWao husema, ‘Je, hivi karibuni hautakuwa wakati wa kujenga nyumba? Mji huu ni chungu cha kupikia, nasi ndio nyama.’ 4 dKwa hiyo toa unabii dhidi yao, tabiri, Ewe mwanadamu.”5 eKisha Roho wa Bwana akaja juu yangu, naye akaniambia niseme: “Hili ndilo Bwana asemalo: Hili ndilo ninyi mnalosema, ee nyumba ya Israeli, lakini ninajua mnalowaza mioyoni mwenu. 6 fMmewaua watu wengi katika mji huu na kujaza barabara zake maiti.
7 g“Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: maiti ulizozitupa huko ni nyama na mji huu ni chungu, lakini nitawaondoa mtoke huko. 8 hMnaogopa upanga, nao upanga huo ndio nitakaouleta juu yenu, asema Bwana Mwenyezi. 9 iNitawaondoa mtoke katika mji na kuwatia mikononi mwa wageni nami nitawaadhibu. 10 jMtaanguka kwa upanga, nami nitatimiza hukumu dhidi yenu katika mipaka ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana. 11 kMji huu hautakuwa chungu kwa ajili yenu, wala hamtakuwa nyama ndani yake. Nitatoa hukumu dhidi yenu katika mipaka ya Israeli. 12 lNanyi mtajua ya kuwa Mimi ndimi Bwana, kwa kuwa hamkufuata amri zangu wala kuzishika sheria zangu, bali mmefuata mwenendo wa mataifa yanayowazunguka.”
13 mBasi nilipokuwa ninatoa unabii, Pelatia mwana wa Benaya akafa. Ndipo nikaanguka kifudifudi, nikalia kwa sauti kuu nikasema, “Ee Bwana Mwenyezi! Je utaangamiza kabisa mabaki ya Israeli?”
14Neno la Bwana likanijia kusema: 15 n“Mwanadamu, ndugu zako, ndugu zako ambao ni wa uhusiano wa damu na nyumba yote ya Israeli, ndio wale ambao watu wa Yerusalemu wamesema, ‘Wako mbali na Bwana; nchi hii tulipewa sisi kuwa milki yetu.’
Ahadi Ya Kurudi Kwa Israeli
16 o“Kwa hiyo sema, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ingawa niliwapeleka mbali miongoni mwa mataifa na kuwatawanya katika nchi mbalimbali, lakini kwa kitambo kidogo mimi nimekuwa mahali patakatifu kwao katika nchi walizokwenda.’17 p“Kwa hiyo sema: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitawakusanyeni kutoka mataifa na kuwarudisha kutoka nchi ambazo mmetawanywa, nami nitawarudishia nchi ya Israeli.’
18 q r“Watairudia nchi na kuondoa vinyago vyote vya upotovu na sanamu zote za machukizo. 19 sNitawapa moyo mmoja na kuweka roho mpya ndani yao, nitaondoa kutoka ndani yao moyo wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama. 20 tKisha watafuata amri zangu na kuwa waangalifu kutii sheria zangu. Watakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wao. 21 uLakini kwa wale ambao mioyo yao imeambatana na vinyago vyao vya upotovu na sanamu zao za machukizo, nitaleta juu ya vichwa vyao yale waliyotenda asema Bwana Mwenyezi.”
22 vNdipo wale makerubi, wenye magurudumu pembeni mwao, wakakunjua mabawa yao, nao utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao.
Copyright information for
SwhNEN