‏ Deuteronomy 3:12-22

Mgawanyo Wa Nchi Mashariki Ya Yordani

(Hesabu 32:1-42)

12 aKatika nchi tuliyoiteka wakati ule, niliwapa kabila la Reubeni na Gadi eneo lililoko kaskazini la Aroeri kando ya Bonde la Arnoni, na nusu ya eneo la milima ya Gileadi, pamoja na miji yake. 13 bKisha nusu ya kabila la Manase niliwapa sehemu ya Gileadi iliyobaki pamoja na Bashani yote, ambayo ilikuwa utawala wa Ogu. (Eneo lote la Argobu katika Bashani lilikuwa linajulikana kama nchi ya Warefai. 14 cYairi, mzao wa kabila la Manase, alichukua eneo lote la nchi ya Argobu hadi kufikia mpaka wa Wageshuri na Wamaaka, ukaitwa kwa jina lake; kwa hiyo mpaka leo hii Bashani inaitwa Hawoth-Yairi.) 15 dNikampa Makiri nchi ya Gileadi. 16 eLakini niliwapa Wareubeni na Wagadi eneo kuanzia Gileadi hadi Bonde la Arnoni (katikati ya bonde ulikuwa ndio mpaka), kuelekea mpaka Mto Yaboki, ambao ndio mpaka wa Waamoni. 17 fKwa upande wa magharibi mpaka wao ulikuwa Yordani katika Araba, toka ziwa Galilaya hadi Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi), kwenye miteremko ya Pisga upande wa mashariki.

18 gWakati huo nilikuamuru: “Bwana Mungu wako amekupa nchi hii uimiliki. Lakini ni lazima wanaume wenu wote wenye uwezo, wakiwa wamejiandaa tayari kwa vita, wavuke ngʼambo wakiwatangulia ndugu zako Waisraeli. 19 hLakini wake zenu, watoto wenu na mifugo yenu (kwani najua mnayo mifugo mingi) wanaweza kukaa katika miji niliyowapa, 20 impaka hapo Bwana atakapowapa ndugu zenu kupumzika kama alivyowapa ninyi, wao pia wamiliki ile nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa, ngʼambo ya Yordani. Baada ya hapo, kila mmoja wenu anaweza kurudi kwenye milki niliyowapa.”

Mose Akatazwa Kuvuka Yordani

21Wakati huo nilimwamuru Yoshua, “Umejionea kwa macho yako mwenyewe yale yote ambayo Bwana Mungu wenu amewafanyia wafalme hawa wawili. Bwana atazifanyia falme zote huko mnakokwenda vivyo hivyo. 22 j , kMsiwaogope, Bwana Mungu wenu atapigana kwa ajili yenu.”

Copyright information for SwhNEN