Acts 10:9-32
Maono Ya Petro
9 aSiku ya pili yake, walipokuwa wameukaribia mji, wakati wa adhuhuri, Petro alipanda juu ya nyumba kuomba. 10 bAlipokuwa akiomba akahisi njaa, akatamani kupata chakula. Lakini wakati walikuwa wakiandaa chakula, akalala usingizi mzito sana. 11 cAkaona mbingu zimefunguka na kitu kama nguo kubwa kikishushwa duniani kwa ncha zake nne. 12Ndani yake walikuwepo aina zote za wanyama wenye miguu minne, nao watambaao nchini, na ndege wa angani. 13Ndipo sauti ikamwambia “Petro, ondoka, uchinje na ule.”14 dPetro akajibu, “La hasha Bwana! Sijawahi kamwe kula kitu chochote kilicho najisi.”
15 eIle sauti ikasema naye mara ya pili, “Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.”
16Jambo hili lilitokea mara tatu na ghafula ile nguo ikarudishwa mbinguni.
17 fWakati Petro akiwa bado anajiuliza kuhusu maana ya maono haya, wale watu waliokuwa wametumwa na Kornelio wakaipata nyumba ya Simoni mtengenezaji wa ngozi wakawa wamesimama mbele ya lango. 18Wakabisha hodi na kuuliza kama Simoni aliyeitwa Petro alikuwa anaishi hapo.
19 gWakati Petro akiwa anafikiria juu ya yale maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Simoni, wako watu watatu wanaokutafuta. 20 hInuka na ushuke, usisite kwenda nao kwa kuwa mimi nimewatuma.”
21Petro akashuka na kuwaambia wale watu waliokuwa wametumwa kutoka kwa Kornelio, “Mimi ndiye mnayenitafuta. Mmekuja kwa sababu gani?”
22 iWale watu wakamjibu, “Tumetumwa na Kornelio yule jemadari. Yeye ni mtu mwema anayemcha Mungu, na anaheshimiwa na Wayahudi wote. Yeye ameagizwa na malaika mtakatifu akukaribishe nyumbani kwake, ili asikilize maneno utakayomwambia.” 23 jBasi Petro akawakaribisha wakafuatana naye ndani, akawapa pa kulala. Kesho yake akaondoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu kutoka Yafa wakafuatana naye.
Petro Nyumbani Mwa Kornelio
24 kSiku iliyofuata wakawasili Kaisaria. Kornelio alikuwa akiwangoja pamoja na jamaa yake na marafiki zake wa karibu. 25Petro alipokuwa akiingia ndani, Kornelio alikuja kumlaki, akaanguka miguuni pake kwa heshima. 26 lLakini Petro akamwinua akamwambia, “Simama, mimi ni mwanadamu tu.”27Petro alipokuwa akizungumza naye akaingia ndani na kukuta watu wengi wamekusanyika. 28 mAkawaambia, “Mnajua kabisa kwamba ni kinyume cha sheria yetu Myahudi kuchangamana na mtu wa Mataifa au kumtembelea. Lakini Mungu amenionyesha kwamba nisimwite mtu yeyote kuwa najisi au asiye safi. 29Ndiyo sababu ulipotuma niitwe nilikuja bila kupinga lolote. Basi sasa naomba unieleze kwa nini umeniita?”
30 nKornelio akajibu, “Siku nne zilizopita, nilikuwa nyumbani nikisali saa kama hii, saa tisa alasiri. Ghafula mtu aliyevaa nguo zilizongʼaa akasimama mbele yangu, 31 oakasema, ‘Kornelio, maombi yako yamesikiwa na sadaka zako kwa maskini zimekumbukwa mbele za Mungu. 32Basi tuma watu waende Yafa wakaulize mtu mmoja Simoni aitwaye Petro, yeye ni mgeni katika nyumba ya Simoni mtengenezaji ngozi, ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.’
Copyright information for
SwhNEN