‏ 2 Kings 25:1-10

Kuanguka Kwa Yerusalemu

(2 Nyakati 36:13-21; Yeremia 52:3-30)

1 aHivyo katika mwaka wa tisa wa utawala wa Sedekia, katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli, akiwa na jeshi lake lote, alifanya vita dhidi ya Yerusalemu. Akapiga kambi nje ya mji na kuuzunguka mji pande zote. 2Mji ulizungukwa na jeshi mpaka mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Mfalme Sedekia. 3 bIlipowadia siku ya tisa ya mwezi wa nne, njaa ikazidi kuwa kali sana ndani ya mji, hadi hapakuwa na chakula kwa ajili ya watu. 4 cKisha ukuta wa mji ukavunjwa, na jeshi lote likakimbia. Wakaondoka mjini usiku kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili karibu na bustani ya mfalme, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji. Wakakimbia kuelekea Araba. 5 dLakini jeshi la Wakaldayo likamfuatia mfalme na kumpata katika sehemu tambarare za Yeriko. Askari wake wote wakatengwa naye na kutawanyika, 6 enaye akakamatwa. Akapelekwa kwa mfalme wa Babeli huko Ribla, mahali ambapo hukumu yake ilitangazwa. 7 fWakawaua wana wa Sedekia mbele ya macho yake. Kisha wakayangʼoa macho yake, wakamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli.

8Mnamo siku ya saba ya mwezi wa tano, katika mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babeli, Nebuzaradani jemadari wa askari walinzi wa mfalme, afisa wa mfalme wa Babeli, alikuja Yerusalemu. 9 gAlichoma moto Hekalu la Bwana, jumba la kifalme, na nyumba zote za Yerusalemu. Aliteketeza kila jengo muhimu. 10 hJeshi lote la Wakaldayo, chini ya jemadari wa askari walinzi wa mfalme, walivunja kuta zilizoizunguka Yerusalemu.
Copyright information for SwhNEN