2 Chronicles 32:1-19
Senakeribu Aitishia Yerusalemu
(2 Wafalme 18:13-37; 19:14-19, 35-37; Isaya 36:1-22; 37:8-38)
1 aBaada ya yale yote aliyokuwa amefanya Hezekia kwa uaminifu mkubwa, Senakeribu mfalme wa Ashuru akaja na kuvamia Yuda. Akaizunguka miji yenye ngome kwa jeshi, akifikiri kuiteka iwe yake. 2 bHezekia alipoona kuwa Senakeribu amekuja na kwamba alikusudia kufanya vita juu ya Yerusalemu, 3akafanya shauri na maafisa wake na mashujaa wake juu ya kuzuia maji kutoka chemchemi zilizo nje ya mji, nao wakamsaidia. 4 cUmati mkubwa wa watu ukakusanyika na kuzuia chemchemi zote na vijito vilivyotiririka katika nchi yote, wakisema: “Kwa nini wafalme wa Ashuru waje na kukuta maji tele?” 5 dHezekia akafanya kazi kwa bidii kukarabati sehemu zote zilizokuwa zimebomoka za ukuta na kujenga minara juu yake. Akajenga ukuta mwingine nje ya ule uliokuwepo na kuimarisha Milo ▼▼Milo maana yake Boma la Ngome.
katika Mji wa Daudi. Akatengeneza pia silaha nyingi na ngao. 6 fAkaweka maafisa wa jeshi juu ya watu, wakawakutanisha mbele yake katika uwanja kwenye lango la mji, naye akawatia moyo kwa maneno haya: 7 g“Kuweni hodari na wenye moyo mkuu. Msiogope, msifadhaike wala msikate tamaa kwa sababu ya mfalme wa Ashuru na hili jeshi kubwa lililo pamoja naye, kwa kuwa aliye pamoja nasi ni mkuu kuliko aliye pamoja naye. 8 hKwake uko mkono wa mwili tu, bali kwetu yuko Bwana Mungu wetu kutusaidia na kutupigania vita vyetu.” Nao watu wakatiwa moyo kutokana na maneno aliyowaambia Hezekia mfalme wa Yuda.
9 iHatimaye Senakeribu mfalme wa Ashuru na majeshi yake yote walipokuwa wameuzunguka Lakishi, akawatuma maafisa wake kwenda Yerusalemu wakiwa na ujumbe huu kwa Hezekia mfalme wa Yuda, na kwa watu wote wa Yuda waliokuwako humo, kusema:
10 j“Hili ndilo asemalo Senakeribu mfalme wa Ashuru: Je, mmeweka tumaini lenu wapi, hata mnaendelea kukaa katika Yerusalemu, hali mmezungukwa na jeshi? 11 kHezekia asemapo, ‘Bwana Mungu wetu atatuokoa kutokana na mkono wa mfalme wa Ashuru,’ anawapotosha ninyi, naye atawaacha mfe kwa njaa na kiu. 12Je, si Hezekia mwenyewe aliyeondoa mahali pa juu pa kuabudia miungu pamoja na madhabahu zake, akiwaambia Yuda wa Yerusalemu, ‘Ni lazima mwabudu mbele ya madhabahu moja na kuteketeza dhabihu juu yake’?
13 l“Je, hamjui yale mimi na baba zangu tuliyoyafanya kwa mataifa yote ya nchi zingine? Je, miungu ya mataifa hayo iliweza kuokoa nchi zao kutoka mkononi mwangu? 14Ni yupi miongoni mwa miungu yote ya mataifa haya ambayo baba zangu waliyaangamiza ameweza kuwaokoa watu wake mkononi mwangu? Inawezekanaje basi Mungu wenu kuwaokoa mkononi mwangu? 15 mSasa basi, msikubali Hezekia awadanganye na kuwapotosha namna hii. Msimwamini, kwa kuwa hakuna mungu wa taifa lolote wala wa ufalme wowote aliyeweza kuwaokoa watu wake kutoka mkononi mwangu au mkononi mwa baba zangu. Sembuse huyo mungu wenu atawaokoaje kutoka mkononi mwangu!”
16Maafisa wa Senakeribu wakaendelea kunena dhidi ya Bwana aliye Mungu na dhidi ya mtumishi wake Hezekia. 17 nMfalme pia aliandika barua akimtukana Bwana, Mungu wa Israeli na kusema haya dhidi yake: “Kama vile miungu ya mataifa ya nchi nyingine ilivyoshindwa kuwaokoa watu wao mkononi mwangu, vivyo hivyo Mungu wa Hezekia hataweza kuwaokoa watu wake kutoka mkononi mwangu.” 18 oKisha wakawaita kwa Kiebrania watu wa Yerusalemu waliokuwa juu ya ukuta ili kuwatisha na kuwatia hofu ili waweze kuuteka mji. 19 pWakanena juu ya Mungu wa Yerusalemu kama vile walivyonena juu ya miungu ya mataifa mengine ya dunia ambayo ni kazi ya mikono ya wanadamu.
Copyright information for
SwhNEN