‏ 2 Chronicles 29

Hezekia Mfalme Wa Yuda

(2 Wafalme 18:1-12)

1 aHezekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Abiya binti Zekaria. 2 bAkafanya yaliyo mema machoni pa Bwana kama Daudi baba yake alivyofanya.

3 cKatika mwezi wa kwanza wa mwaka wa kwanza wa utawala wa alifungua milango ya Hekalu la Bwana, na kuikarabati. 4Akawaingiza makuhani na Walawi ndani na kuwakutanisha katika uwanja upande wa mashariki 5 dna kusema: “Nisikilizeni mimi, enyi Walawi! Jitakaseni nafsi zenu sasa, mkaitakase na nyumba ya Bwana, Mungu wa baba zenu. Ondoeni uchafu wote kutoka mahali patakatifu. 6 eBaba zetu hawakuwa waaminifu, walifanya maovu machoni pa Bwana Mungu wetu na wakamwacha yeye. Wakageuza nyuso zao mbali na Maskani ya Bwana wakamgeuzia visogo vyao. 7 fPia walifunga milango ya ukumbi wa Hekalu na kuzima taa zake. Hawakufukiza uvumba wala kutoa sadaka yoyote ya kuteketezwa katika mahali patakatifu kwa Mungu wa Israeli. 8 gKwa hiyo, hasira ya Bwana ikashuka juu ya Yuda na Yerusalemu, naye akawa amewafanya kitu cha kutisha, cha kushangaza na kitu cha kufanyia mzaha kama mnavyoona kwa macho yenu wenyewe. 9 hHii ndiyo sababu baba zetu wameanguka kwa upanga na ndiyo sababu wana wetu na binti zetu, pia wake zetu wamekuwa mateka. 10 iSasa ninadhamiria moyoni mwangu kuweka Agano na Bwana, Mungu wa Israeli, ili hasira yake kali igeuziwe mbali nasi. 11 jWanangu, basi msipuuze jambo hili sasa, kwa kuwa Bwana amewachagua ninyi msimame mbele zake na kumtumikia, mkawe watumishi wake na mkamfukizie uvumba.”

12 kNdipo Walawi wafuatao wakaanza kazi:

Kutoka kwa Wakohathi,
Mahathi mwana wa Amasai na Yoeli mwana wa Azaria;
kutoka kwa Wamerari,
Kishi mwana wa Abdi na Azaria mwana wa Yahaleleli;
kutoka kwa Wagershoni,
Yoa mwana wa Zima na Edeni mwana wa Yoa;
13 lkutoka kwa wana wa Elisafani,
Shimri na Yeieli;
kutoka kwa wana wa Asafu,
Zekaria na Matania;
14kutoka kwa wana wa Hemani,
Yehieli na Shimei;
kutoka kwa wana wa Yeduthuni,
Shemaya na Uzieli.
15 mWalipomaliza kuwakusanya ndugu zao na kujiweka wakfu, wakaingia ndani ili kutakasa Hekalu la Bwana, kama vile mfalme alivyokuwa ameagiza, kwa kufuata neno la Bwana. 16 nMakuhani wakaingia patakatifu pa Hekalu la Bwana ili kupatakasa. Wakatoa nje penye ua wa Hekalu la Mungu kila kitu kichafu walichokikuta kwenye Hekalu la Bwana. Walawi wakavichukua na kuvipeleka nje katika Bonde la Kidroni. 17 oWalianza kazi ya utakaso siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza na kufikia siku ya nane ya mwezi huo wakawa wamefikia kwenye ukumbi wa Bwana. Kwa siku zingine nane wakalitakasa Hekalu lenyewe la Bwana wakakamilisha katika siku ya kumi na sita ya mwezi huo wa kwanza.

18Kisha wakaingia ndani kwa Mfalme Hezekia kutoa habari na kusema: “Tumelitakasa Hekalu lote la Bwana, madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa pamoja na vyombo vyake vyote, meza ya kupanga mikate iliyowekwa wakfu, pamoja na vyombo vyake vyote. 19 pTumeviandaa na kuvitakasa vyombo vyote vile ambavyo Mfalme Ahazi, kwa kukosa uaminifu kwake, aliviondoa wakati alipokuwa mfalme. Sasa viko mbele ya madhabahu ya Bwana.”

Ibada Hekaluni Yarejeshwa

20Ndipo Mfalme Hezekia akainuka asubuhi na mapema, akakusanya pamoja maafisa wa mji wakakwea hekaluni mwa Bwana. 21 qWakaleta mafahali saba, kondoo dume saba, wana-kondoo dume saba na mabeberu saba kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya ufalme, kwa ajili ya mahali patakatifu na kwa ajili ya Yuda. Mfalme akawaamuru makuhani, wazao wa Aroni, kuvitoa vitu hivyo sadaka katika madhabahu ya Bwana. 22 rHivyo wakachinja wale mafahali, nao makuhani wakachukua ile damu na kuinyunyiza kwenye madhabahu, halafu wakawachinja wale kondoo dume saba na kunyunyiza hiyo damu yao kwenye madhabahu, kisha wakawachinja wale wana-kondoo dume na kunyunyiza damu yao kwenye madhabahu. 23 sWale mabeberu waliokuwa kwa ajili ya sadaka ya dhambi wakaletwa mbele ya mfalme na kusanyiko nao wakaweka mikono yao juu hao mabeberu. 24 tNdipo makuhani wakawachinja hao mabeberu na kuweka damu yao kwenye madhabahu kwa ajili ya sadaka ya dhambi ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Israeli yote, kwa sababu mfalme alikuwa ameamuru hiyo sadaka ya kuteketezwa na hiyo sadaka ya dhambi kwa ajili ya Israeli yote.

25 uAkawaweka Walawi kwenye Hekalu la Bwana wakiwa na matoazi, vinubi na zeze kama ilivyoagizwa na Daudi na Gadi mwonaji wa mfalme pamoja na nabii Nathani kwani hili lilikuwa limeamriwa na Bwana kupitia manabii wake. 26 vHivyo Walawi wakasimama tayari wakiwa na ala za uimbaji za Daudi na makuhani walikuwa na tarumbeta zao.

27 wHezekia akatoa amri ya kutoa sadaka ya kuteketezwa madhabahuni. Walipoanza kutoa sadaka, wakaanza pia kumwimbia Bwana pamoja na tarumbeta na zile ala za uimbaji za Daudi mfalme wa Israeli. 28Kusanyiko lote wakaabudu kwa kusujudu, wakati waimbaji wakiwa wanaimba na wenye tarumbeta wakipiga tarumbeta zao. Yote haya yaliendelea mpaka walipomaliza kutoa ile dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa.

29 xKutoa sadaka kulipomalizika, mfalme na kila mtu aliyekuwepo pamoja naye wakapiga magoti na kuabudu. 30 yMfalme Hezekia na maafisa wake wakawaamuru Walawi kumsifu Bwana kwa maneno ya Daudi na ya Asafu mwonaji. Hivyo wakaimba sifa kwa furaha nao wakainamisha vichwa vyao na kuabudu.

31 zKisha Hezekia akasema, “Sasa mmejiweka wakfu kwa Bwana. Njooni mlete dhabihu na sadaka za shukrani Hekaluni mwa Bwana.” Hivyo kusanyiko likaleta dhabihu na sadaka za shukrani, nao wote waliokuwa na mioyo ya hiari wakaleta sadaka za kuteketezwa.

32Idadi ya sadaka za kuteketezwa zilizoletwa na kusanyiko zilikuwa mafahali sabini, kondoo dume 100 na wana-kondoo dume 200. Wote hawa walikuwa kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa kwa Bwana. 33Wanyama waliowekwa wakfu kwa sadaka ya kuteketezwa walikuwa mafahali 600, pamoja na kondoo na mbuzi 3,000. 34 aaLakini makuhani walikuwa wachache sana kuweza kuchuna wale wanyama wote wa sadaka za kuteketezwa, kwa hiyo ndugu zao Walawi wakawasaidia mpaka kazi ile ikakamilika na mpaka makuhani wengine walipowekwa wakfu, kwa kuwa Walawi walikuwa makini kujiweka wakfu kuliko walivyokuwa makuhani. 35 abKulikuwa na sadaka nyingi za kuteketezwa, pamoja na mafuta ya wanyama ya sadaka za amani na sadaka za kinywaji ambazo ziliambatana na sadaka za kuteketezwa.

Kwa hiyo huduma ya Hekalu la Bwana ikarudishwa kwa upya.
36 acHezekia pamoja na watu wote wakafurahi kwa sababu ya lile Mungu alilolifanya kwa ajili ya watu wake, kwa kuwa lilitendeka papo hapo.

‏ 2 Chronicles 30

Hezekia Aadhimisha Pasaka

1 adHezekia akatuma ujumbe kuwaita Israeli wote na Yuda, pia akaandika barua kwa Efraimu na Manase, kuwakaribisha ili waje hekaluni mwa Bwana huko Yerusalemu kuadhimisha Pasaka kwa Bwana, Mungu wa Israeli. 2 aeMfalme na maafisa wake pamoja na kusanyiko lote katika Yerusalemu waliamua kuadhimisha Pasaka katika mwezi wa pili. 3 afKwa sababu makuhani hawakuwa wamejitakasa idadi ya kutosha na watu wakawa hawajakusanyika huko Yerusalemu, hawakuwa wameweza kuadhimisha Pasaka kwa wakati wake wa kawaida. 4Mpango huu ukaonekana wafaa kwa mfalme na kusanyiko lote. 5 agWakaamua kupeleka tangazo Israeli kote, kuanzia Beer-Sheba hadi Dani, wakiwaita watu waje Yerusalemu kuadhimisha Pasaka ya Bwana, Mungu wa Israeli. Ilikuwa haijaadhimishwa na idadi kubwa ya watu kama hiyo kufuatana na yale yaliyokuwa yameandikwa.

6 ahKwa amri ya mfalme, matarishi wakapita katika Israeli na Yuda kote wakiwa na barua kutoka kwa mfalme na kutoka kwa maafisa wake zikisema:

“Watu wa Israeli, mrudieni Bwana, Mungu wa Abrahamu, Isaki na Israeli, ili naye awarudie ninyi mliosalia, mlionusurika kutoka mikononi mwa wafalme wa Ashuru.
7 aiMsiwe kama baba zenu na ndugu zenu, ambao hawakuwa waaminifu kwa Bwana, Mungu wa baba zao, hivyo akawafanya kitu cha kushangaza kama mnavyoona. 8 ajMsiwe na shingo ngumu, kama baba zenu walivyokuwa, bali nyenyekeeni kwa Bwana. Njooni mahali patakatifu, alipopatakasa milele. Mtumikieni Bwana Mungu wenu, ili hasira yake kali igeuziwe mbali nanyi. 9 akKama mkimrudia Bwana ndipo wale ndugu zenu waliotekwa pamoja na watoto wenu watakapoonewa huruma na wale waliowateka na kuwaachia warudi katika nchi hii, kwa kuwa Bwana Mungu wenu ni mwenye neema na huruma, hatageuzia uso wake mbali nanyi kama ninyi mkimrudia yeye.”

10 alMatarishi wakaenda mji hadi mji katika Efraimu na Manase, wakafika mpaka Zabuloni, lakini watu wakawadharau na kuwadhihaki. 11 amLakini, baadhi ya watu wa Asheri, Manase na Zabuloni, wakajinyenyekeza wakaja Yerusalemu. 12 anPia katika Yuda mkono wa Mungu ulikuwa juu ya watu kuwapa umoja katika kutenda yale ambayo mfalme na maafisa wake waliwaamuru, kulingana na neno la Bwana.

13 aoBasi umati mkubwa wa watu ukakusanyika huko Yerusalemu kuadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu katika mwezi wa pili. 14 apWakajitia kazini kuyaondoa yale madhabahu yaliyokuwa huko Yerusalemu, wakayaondoa pia yale madhabahu ya kufukizia uvumba kwa miungu na kuyatupa Bonde la Kidroni.

15 aqKisha wakamchinja mwana-kondoo wa Pasaka katika siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili. Makuhani na Walawi waliona aibu, wakajitakasa na kuleta sadaka za kuteketezwa katika Hekalu la Bwana. 16 arKisha wakachukua nafasi zao za kawaida kama ilivyoelezwa katika Sheria ya Mose mtu wa Mungu. Makuhani wakanyunyiza ile damu waliyokabidhiwa na Walawi. 17 asKwa kuwa wengi waliokuwa katika lile kusanyiko walikuwa hawajajitakasa, iliwapasa Walawi wachinje wana-kondoo wengine wa Pasaka kwa ajili ya wale watu ambao hawakuwa safi, kwa kufuata taratibu za ibada ili kuwatakasa kwa Bwana. 18 atIngawa watu wengi miongoni mwa wale waliotoka Efraimu, Manase, Isakari na Zabuloni walikuwa hawajajitakasa, hata hivyo walikula Pasaka kinyume na ilivyoandikwa. Lakini Hezekia akawaombea, akisema, “Bwana, ambaye ni mwema na amsamehe kila mmoja 19 auambaye anauelekeza moyo wake kumtafuta Mungu, Bwana, Mungu wa baba zake, hata kama yeye si safi kulingana na sheria za mahali patakatifu.” 20 avNaye Bwana akamsikia Hezekia akawaponya watu.

21 awWaisraeli waliokuwa Yerusalemu wakaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu kwa muda wa siku saba, nao Walawi na makuhani walikuwa wakiimba kila siku, wakiwa na ala za uimbaji za kumsifu Bwana.

22 axHezekia akazungumza akiwatia moyo Walawi wote, ambao walionyesha ustadi katika kumtumikia Bwana. Hivyo watu wakala chakula cha sikukuu kwa siku saba, wakitoa sadaka za amani na kumshukuru Bwana, Mungu wa baba zao.

23 ayKisha kusanyiko lote likakubali kuendelea na sikukuu kwa siku saba zaidi, kwa hiyo kwa siku saba nyingine wakaendelea kuiadhimisha kwa furaha. 24 azHezekia, mfalme wa Yuda akatoa mafahali 1,000, kondoo na mbuzi 7,000 kwa ajili ya kusanyiko, nao maafisa wakatoa mafahali 1,000 pamoja na kondoo na mbuzi 10,000. Idadi kubwa ya makuhani wakajiweka wakfu. 25 baKusanyiko lote la Yuda, pamoja na makuhani na Walawi na lile kusanyiko lote lililotoka Israeli, pamoja na wale wageni waliotoka Israeli na wale walioishi katika Yuda wakafurahi. 26Kulikuwa na furaha kubwa katika Yerusalemu, kwa sababu tangu siku za Mfalme Solomoni mwana wa Daudi mfalme wa Israeli halijakuwepo jambo kama hili katika Yerusalemu. 27 bbNdipo makuhani na Walawi wakasimama wakawabariki watu, naye Mungu akawasikia, kwa sababu maombi yao yalifika mbinguni, makao yake matakatifu.

‏ 2 Chronicles 31

Sehemu Za Ibada Za Kipagani Zaondolewa

1 bcBaada ya mambo haya yote kumalizika, Waisraeli ambao walikuwako huko wakaenda kwenye miji ya Yuda, wakayavunja yale mawe ya kuabudia na kuzikatakata zile nguzo za Ashera. Wakabomoa mahali pa juu pa kuabudia miungu pamoja na madhabahu zake kila mahali katika Yuda na Benyamini na katika Efraimu na Manase. Baada ya kuviharibu hivi vyote, Waisraeli wakarudi katika miji yao wenyewe na kwenye milki zao.

2 bdHezekia akawapanga makuhani na Walawi katika migawanyo, kila mgawanyo kulingana na wajibu wao, kama ni makuhani au Walawi, ili kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, kuhudumu, kushukuru na kuimba sifa katika malango ya makao ya Bwana. 3 beMfalme akatoa matoleo kutoka mali zake mwenyewe kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa za asubuhi na za jioni na sadaka za kuteketezwa kwa siku za Sabato, kwa Sikukuu za Mwezi Mwandamo na kwa ajili ya sikukuu zilizoamriwa kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Bwana. 4 bfAkawaagiza watu wanaoishi Yerusalemu watoe sehemu iliyo haki ya makuhani na Walawi ili waweze kujitoa kikamilifu kutimiza wajibu wao katika Sheria ya Bwana. 5 bgMara tu baada ya kutolewa tangazo hilo, Waisraeli wakatoa kwa ukarimu malimbuko ya nafaka zao, divai mpya, mafuta na asali pamoja na vyote vilivyotoka mashambani. Wakaleta kiasi kikubwa cha fungu la kumi la kila kitu. 6 bhWatu wa Israeli na Yuda walioishi katika miji ya Yuda wakaleta pia fungu la kumi la makundi yao ya ngʼombe na makundi ya kondoo na mbuzi pia na fungu la kumi la vitu vitakatifu vilivyowekwa wakfu kwa ajili ya Bwana Mungu wao na kuvikusanya katika malundo. 7 biWakaanza kufanya haya katika mwezi wa tatu na kumaliza katika mwezi wa saba. 8 bjWakati Hezekia na maafisa wake walipokuja na kuona yale malundo, wakamsifu Bwana na kuwabariki watu wake Israeli.

9Hezekia akawauliza makuhani na Walawi kuhusu yale malundo, 10 bknaye Azaria aliyekuwa kuhani mkuu, kutoka jamaa ya Sadoki, akajibu, “Tangu watu walipoanza kuleta sadaka zao katika Hekalu la Bwana tumekuwa na chakula cha kutosha na vingi vya kuweka akiba kwa sababu Bwana amewabariki watu wake, hivyo tumekuwa na kiasi kingi kilichobaki.”

Kutambuliwa Kwa Makuhani Na Walawi

11Hezekia akatoa agizo la kutengeneza vyumba vya ghala katika Hekalu la Bwana nalo hili likafanyika. 12 blKisha kwa uaminifu wakaleta sadaka zao, mafungu yao ya kumi na vitu vilivyowekwa wakfu. Konania Mlawi, ndiye alikuwa msimamizi wa vitu hivi na Shimei ndugu yake ndiye alikuwa msaidizi wake. 13Yehieli, Azazia, Nahathi, Asaheli, Yeremothi, Yozabadi, Elieli, Ismakia, Mahathi na Benaya walikuwa waangalizi chini ya Konania na Shimei ndugu yake, waliokuwa wamewekwa na Mfalme Hezekia na Azaria, afisa msimamizi wa Hekalu la Mungu.

14Kore mwana wa Imna, Mlawi, bawabu wa Lango la Mashariki, alikuwa msimamizi wa sadaka za hiari zilizotolewa kwa Mungu, akiyagawanya hayo matoleo yaliyotolewa kwa Bwana na pia zile sadaka zilizowekwa wakfu. 15 bmEdeni, Miniamini, Yeshua, Shemaya, Amaria na Shekania walimsaidia kwa uaminifu katika miji ya makuhani, wakiwagawia makuhani wenzao kufuatana na migawanyo yao, wazee kwa vijana sawasawa.

16 bnZaidi ya hao wakawagawia wanaume wenye umri wa miaka mitatu au zaidi ambao majina yao yalikuwa kwenye orodha ya vizazi, wale wote ambao wangeingia katika Hekalu la Bwana ili kufanya kazi zao mbalimbali za kila siku kulingana na wajibu katika mgawanyo wao. 17 boKuandikishwa kwa makuhani kulikuwa kwa kufuata chimbuko la nyumba za baba zao na Walawi kuanzia umri wa miaka ishirini au zaidi ilikuwa kufuatana na huduma zao, kwa migawanyo yao. 18Makuhani waliandikishwa pamoja na watoto wao wadogo, wake zao, watoto wao wa kiume na wa kike, jamii yote iliandikishwa kwa kufuata orodha ya vizazi vyao. Kwa kuwa walikuwa waaminifu katika kujitakasa.

19 bpKuhusu makuhani, wazao wa Aroni walioishi kwenye mashamba yaliyozunguka miji yao au katika miji mingine yoyote, watu walitajwa majina ili kumgawia kila mwanaume miongoni mwao na kwa wote waliokuwa katika orodha ya vizazi vya Walawi.

20 bqHivi ndivyo Hezekia alivyofanya katika Yuda yote, akifanya lile lililo jema, sawa na la uaminifu mbele za Bwana Mungu wake. 21 brNaye katika kila kitu alichofanya katika huduma kwenye Hekalu la Mungu na katika utii kwa sheria na amri, alimtafuta Mungu wake na kufanya kazi kwa moyo wake wote. Naye hivyo akafanikiwa.

Copyright information for SwhNEN