‏ 1 Kings 8:9-21

9Ndani ya Sanduku hapakuwepo kitu kingine chochote isipokuwa zile mbao mbili za mawe ambazo Mose alikuwa ameziweka ndani yake huko Horebu, mahali ambapo Bwana alifanya Agano na Waisraeli baada ya kutoka Misri.

10Makuhani walipoondoka katika Mahali Patakatifu, wingu likajaza Hekalu la Bwana. 11Nao makuhani hawakuweza kufanya huduma yao kwa sababu ya lile wingu, kwa kuwa utukufu wa Bwana ulijaza Hekalu lake.

12Ndipo Solomoni akasema, “Bwana alisema kwamba ataishi katika giza nene; 13 anaam, hakika nimekujengea Hekalu zuri sana, mahali pako pa kuishi milele.”

Hotuba Ya Solomoni

(2 Nyakati 6:3-11)

14Kusanyiko lote la Israeli lilipokuwa limesimama hapo, mfalme akageuka na kuwabariki. 15 bKisha akasema:

“Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye kwa mkono wake mwenyewe ametimiza lile alilomwahidi Daudi baba yangu kwa kinywa chake mwenyewe. Kwa kuwa alisema,
16‘Tangu siku niliyowatoa watu wangu Israeli kutoka Misri, sikuchagua mji katika kabila lolote la Israeli ili Hekalu lijengwe humo ili Jina langu lipate kuwamo humo, bali nimemchagua Daudi kuwatawala watu wangu Israeli.’

17 c“Ilikuwa moyoni mwa Daudi baba yangu kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Bwana, Mungu wa Israeli. 18 dLakini Bwana akamwambia Daudi baba yangu, ‘Kwa sababu ilikuwa moyoni mwako kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu, ulifanya vyema kuwa na jambo hili moyoni mwako. 19Hata hivyo, sio wewe utakayenijengea hekalu, bali mwanao, ambaye ni nyama yako na damu yako mwenyewe, yeye ndiye atakayejenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’

20 eBwana ametimiza ahadi aliyoiweka: Nimeingia mahali pa Daudi baba yangu na sasa ninakikalia kiti cha ufalme cha Israeli, kama vile Bwana alivyoahidi, nami nimejenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Bwana, Mungu wa Israeli. 21 f , gNimetenga nafasi humo kwa ajili ya Sanduku la Agano, ambamo ndani yake kuna lile Agano la Bwana alilofanya na baba zetu wakati alipowatoa Misri.”

Copyright information for SwhNEN