‏ 1 Kings 17:8-16

8Kisha neno la Bwana likamjia, kusema, 9 a“Ondoka, uende Sarepta ya Sidoni na ukae huko. Nimemwagiza mjane katika sehemu ile akupatie chakula.” 10 bHivyo akaenda Sarepta. Alipofika kwenye lango la mji, mjane alikuwa huko akiokota kuni. Akamwita na kumwambia, “Naomba uniletee maji kidogo kwenye gudulia ili niweze kunywa.” 11Alipokuwa anakwenda kumletea, akamwita akasema, “Tafadhali niletee pia kipande cha mkate.”

12 cAkamjibu, “Hakika kama Bwana Mungu wako aishivyo, sina mkate wowote, isipokuwa konzi ya unga kwenye gudulia na mafuta kidogo kwenye chupa. Ninakusanya kuni chache nipeleke nyumbani na nikapike chakula kwa ajili yangu na mwanangu, ili kwamba tule, kiishe, tukafe.”

13Eliya akamwambia, “Usiogope. Nenda nyumbani ukafanye kama ulivyosema. Lakini kwanza unitengenezee mimi mkate mdogo kutoka vile ulivyo navyo kisha uniletee na ndipo utayarishe chochote kwa ajili yako na mwanao. 14Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Lile gudulia la unga halitakwisha wala ile chupa ya mafuta haitakauka hadi siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi.’ ”

15Akaondoka na kufanya kama Eliya alivyomwambia. Kwa hiyo kukawa na chakula kila siku kwa ajili ya Eliya, yule mwanamke na jamaa yake. 16Kwa kuwa lile gudulia la unga halikwisha na ile chupa ya mafuta haikukauka, sawasawa na lile neno la Bwana alilosema Eliya.

Copyright information for SwhNEN