1 Chronicles 17:1-15
Ahadi Ya Mungu Kwa Daudi
(2 Samweli 7:1-17)
1 aBaada ya Daudi kuingia rasmi katika jumba lake la kifalme, akamwambia nabii Nathani, “Hebu tazama, mimi ninakaa kwenye nyumba nzuri iliyojengwa kwa mierezi, wakati Sanduku la Agano la Bwana liko ndani ya hema.”2 bNathani akamjibu Daudi, “Lolote ulilo nalo moyoni mwako litende, kwa maana Mungu yu pamoja nawe.” 3Usiku ule neno la Mungu likamjia Nathani, kusema:
4 c“Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Wewe hutanijengea mimi nyumba ili nikae humo. 5 dMimi sijakaa ndani ya nyumba tangu siku ile niliyowatoa Israeli kutoka Misri mpaka leo. Nimehama kutoka hema moja hadi jingine na kutoka mahali pamoja hadi pengine. 6Je, popote nilipokwenda pamoja na Waisraeli wote, wakati wowote nilimwambia kiongozi yeyote niliyemwagiza kuwachunga watu wangu, kwa nini hujanijengea nyumba ya mierezi?’
7 e“Sasa basi, mwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: Nilikuchukua machungani na kutoka kuandama kondoo ili uwatawale watu wangu Israeli. 8Nimekuwa pamoja nawe popote ulipokwenda, nami nimekuondolea mbali adui zako wote mbele yako. Basi nitalifanya jina lako kuwa kuu kama majina ya watu walio wakuu sana duniani. 9 fNami nitawapatia watu wangu Israeli mahali na nitawapa ili wawe na mahali pao wenyewe pa kuishi na wasisumbuliwe tena. Watu waovu hawatawaonea tena, kama walivyofanya mwanzoni, 10 gna ambavyo wamefanya siku zote tangu nilipowachagua viongozi kwa ajili ya watu wangu Israeli. Pia nitawatiisha adui zenu wote.
“ ‘Pamoja na hayo ninakuambia kwamba Bwana atakujengea nyumba: 11Wakati wako utakapokuwa umekwisha, nawe ukawa umekwenda kukaa na baba zako, nitamwinua mzao wako aingie mahali pako kuwa mfalme, mmoja wa wana wako mwenyewe, nami nitaufanya imara ufalme wake. 12 hYeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili yangu, nami nitakifanya imara kiti cha ufalme wake milele. 13 iMimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Kamwe sitaondoa upendo wangu kwake, kama nilivyouondoa kwa yeye aliyekutangulia. 14 jNitamweka juu ya nyumba yangu na ufalme wangu milele; kiti chake cha enzi nitakifanya imara milele.’ ”
15Nathani akamwarifu Daudi maneno yote ya maono haya.
Copyright information for
SwhNEN