‏ Titus 2

Fundisha Mafundisho Manyofu

1 aInakupasa kufundisha itikadi sahihi. 2 bWafundishe wazee kuwa na kiasi, wastahivu, wenye busara na wanyofu katika imani, upendo na saburi.

3 cVivyo hivyo, wafundishe wanawake wazee kuwa na mwenendo wa utakatifu, wala wasiwe wasingiziaji au walevi, bali wafundishe yale yaliyo mema, 4 dili waweze kuwafundisha wanawake vijana kuwa na kiasi, wawapende waume zao na kuwapenda watoto wao, 5 ewawe waaminifu, watakatifu, wakitunza vyema nyumba zao, wema, watiifu kwa waume zao, ili mtu yeyote asije akalikufuru neno la Mungu.

6 fVivyo hivyo, himiza vijana wawe na kiasi. 7 gKatika kila jambo uwe kielelezo kwa kutenda mema. Katika mafundisho yako uonyeshe uadilifu, utaratibu, 8 hna usemi sahihi usio na lawama, ili wanaokupinga watahayari, wakose neno lolote baya la kusema juu yetu.

9 iWafundishe watumwa kuwatii mabwana zao katika kila jambo, wakijitahidi kuwapendeza wala wasijibizane nao, 10 jwala wasiwaibie, bali waonyeshe kuwa wanaweza kuaminika kabisa, ili kwa kila namna wayafanye mafundisho ya Mungu Mwokozi wetu yawe ya kuvutia.

11 kKwa maana neema ya Mungu ambayo inawaokoa wanadamu wote imefunuliwa. 12 lNayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia, ili tupate kuishi maisha ya kiasi, ya haki na ya utaua katika ulimwengu huu wa sasa, 13 mhuku tukilitazamia tumaini lenye baraka na ufunuo wa utukufu wa Mungu wetu Mkuu, aliye Mwokozi wetu Yesu Kristo. 14 nNdiye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe kutoka uovu wote na kujisafishia watu kuwa mali yake Mwenyewe, yaani, wale walio na juhudi katika kutenda mema.

15Basi wewe fundisha mambo haya. Onya na kukaripia kwa mamlaka yote. Mtu yeyote asikudharau.

Copyright information for SwhNEN