Revelation of John 10
Malaika Mwenye Kitabu Kidogo
1 aKisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu na upinde wa mvua juu ya kichwa chake. Uso wake ulingʼaa kama jua na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto. 2 bMkononi mwake alikuwa ameshika kijitabu kilichokuwa kimefunguliwa. Akauweka mguu wake wa kuume juu ya bahari na mguu wake wa kushoto akauweka juu ya nchi kavu. 3 cNaye akapiga kelele kwa sauti kuu kama simba anayenguruma. Alipopiga kelele, zile radi saba zikatoa ngurumo zake. 4 dNazo zile radi saba zilipotoa ngurumo, nilitaka kuanza kuandika, lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Yatie muhuri hayo yaliyosemwa na hizo radi saba na usiyaandike.”5 eKisha yule malaika niliyekuwa nimemwona akiwa amesimama juu ya bahari na juu ya nchi akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni. 6 fNaye akaapa kwa Yule aishiye milele na milele, aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, dunia na vyote viijazavyo, pamoja na bahari na vyote vilivyomo ndani yake, akasema, “Hakuna kungoja tena! 7 gLakini katika siku zile ambazo huyo malaika wa saba atakapokaribia kuipiga hiyo tarumbeta yake, siri ya Mungu itatimizwa, kama vile alivyowatangazia watumishi wake manabii.”
8Ndipo ile sauti niliyokuwa nimeisikia kutoka mbinguni ikasema nami tena ikaniambia, “Nenda, chukua kile kitabu kilichofunguliwa kilichoko mkononi mwa yule malaika aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu.”
9 hBasi nikamwendea nikamwomba yule malaika anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, “Chukua na ukile. Kitakuwa kichungu tumboni mwako, lakini kinywani mwako kitakuwa kitamu kama asali.” 10 iHivyo nikakichukua kile kitabu kidogo kutoka mkononi mwa yule malaika nikakila. Kilikuwa kitamu kama asali kinywani mwangu, lakini baada ya kukila, tumbo langu likatiwa uchungu. 11 jKisha nikaambiwa, “Imekupasa kutoa unabii tena kuhusu makabila mengi, mataifa, lugha na wafalme.”
Copyright information for
SwhNEN