‏ Psalms 42

KITABU CHA PILI

(Zaburi 42–72)

Maombi Ya Mtu Aliye Uhamishoni

Kwa mwimbishaji. Utenzi wa wana wa Kora.

1 aKama vile ayala aoneavyo shauku vijito vya maji,
ndivyo nafsi yangu ikuoneavyo shauku, Ee Mungu.
2 bNafsi yangu inamwonea Mungu kiu, Mungu aliye hai.
Ni lini nitaweza kwenda kukutana na Mungu?
3 cMachozi yangu yamekuwa chakula changu
usiku na mchana,
huku watu wakiniambia mchana kutwa,
“Yuko wapi Mungu wako?”
4 dMambo haya nayakumbuka
ninapoimimina nafsi yangu:
Jinsi nilivyokuwa nikienda na umati wa watu,
nikiongoza maandamano kuelekea kwenye nyumba ya Mungu,
kwa kelele za shangwe na za shukrani
katikati ya umati uliosherehekea.

5 eEe nafsi yangu, kwa nini unasononeka?
Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu?
Weka tumaini lako kwa Mungu,
kwa sababu bado nitamsifu,
Mwokozi wangu na
6 fMungu wangu.

Nafsi yangu inasononeka ndani yangu;
kwa hiyo nitakukumbuka
kutoka nchi ya Yordani,
katika vilele vya Hermoni,
kutoka Mlima Mizari.
7 gKilindi huita kilindi,
katika ngurumo za maporomoko ya maji yako;
mawimbi yako yote pamoja na viwimbi
vimepita juu yangu.

8 hMchana Bwana huelekeza upendo wake,
usiku wimbo wake uko nami:
maombi kwa Mungu wa uzima wangu.

9 iNinamwambia Mungu Mwamba wangu,
“Kwa nini umenisahau?
Kwa nini niendelee kuomboleza,
nikiwa nimeonewa na adui?”
10 jMifupa yangu inateseka kwa maumivu makali
adui zangu wanaponidhihaki,
wakiniambia mchana kutwa,
“Yuko wapi Mungu wako?”

11 kEe nafsi yangu, kwa nini unasononeka?
Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu?
Weka tumaini lako kwa Mungu,
kwa sababu bado nitamsifu,
Mwokozi wangu na Mungu wangu.
Copyright information for SwhNEN