‏ Numbers 18

Wajibu Wa Makuhani Na Walawi

1 a Bwana akamwambia Aroni, “Wewe, wanao na jamaa ya baba yako mtawajibika kwa makosa dhidi ya mahali patakatifu, na wewe na wanao peke yenu ndio mtakaowajibika kwa makosa dhidi ya ukuhani. 2 bWalete Walawi wenzako kutoka kabila la baba zako ili waungane nanyi na kuwasaidia wakati wewe na wanao mnapohudumu mbele ya Hema la Ushuhuda. 3 cWatawajibika kwenu na watafanya kazi zote za Hema, lakini kamwe wasisogelee vifaa vya patakatifu au madhabahu, la sivyo wao na ninyi mtakufa. 4 dWatajiunga nanyi na watawajibika kwa utunzaji wa Hema la Kukutania, yaani kazi zote kwenye Hema, wala hakuna mtu mwingine yeyote atakayeweza kusogea karibu hapo mlipo.

5 e“Mtawajibika katika utunzaji wa mahali patakatifu na madhabahu, ili kwamba ghadhabu isiwaangukie Waisraeli tena. 6 fMimi mwenyewe nimewachagua Walawi wenzenu kutoka miongoni mwa Waisraeli kama zawadi kwenu, waliowekwa wakfu kwa Bwana ili kufanya kazi katika Hema la Kukutania. 7 gLakini ni wewe tu na wanao mtakaoweza kutumika kama makuhani kuhusiana na kila kitu kwenye madhabahu na ndani ya pazia. Ninawapa utumishi wa ukuhani kama zawadi. Mtu mwingine yeyote atakayekaribia mahali patakatifu ni lazima auawe.”

Sadaka Kwa Ajili Ya Makuhani Na Walawi

8 hKisha Bwana akamwambia Aroni, “Mimi mwenyewe nimekuweka kuwa mwangalizi wa sadaka zote zitakazotolewa kwangu; matoleo yote matakatifu Waisraeli wanayonipa ninakupa wewe na wanao kama sehemu yenu na fungu lenu la kawaida. 9 iMtachukua sehemu ya yale matoleo matakatifu sana ambayo hayateketezwi kwa moto. Kutoka kwa matoleo yote wanayoniletea kama sadaka takatifu sana, ziwe za nafaka, au za dhambi, au za makosa, sehemu ile itakuwa yako na wanao. 10 jMtaila kama kitu kilicho kitakatifu sana; kila mwanaume ataila. Ni lazima mtaiheshimu kama takatifu.

11 k“Hiki pia ni chako: chochote kilichotengwa kutoka kwenye matoleo yote ya sadaka za kuinuliwa za Waisraeli. Ninakupa wewe haya, wana na binti zako kama sehemu yenu ya kawaida. Kila mmoja wa nyumba yako ambaye ni safi kwa taratibu za ibada anaweza kuyala.

12 l“Ninawapa mafuta ya zeituni yaliyo bora kuliko yote, na divai mpya iliyo bora kuliko zote na nafaka wanazompa Bwana kama malimbuko katika mavuno yao. 13 mMalimbuko yote ya nchi ambayo wanamletea Bwana yatakuwa yenu. Kila mmoja nyumbani kwako ambaye ni safi kwa taratibu za Ibada anaweza kula.

14 n“Kila kitu katika Israeli ambacho kimetolewa kwa Bwana ni chenu. 15 oKila mzaliwa wa kwanza wa mwanadamu na wa mnyama, ambaye ametolewa kwa Bwana ni wenu. Lakini ni lazima mtamkomboa kila mwana mzaliwa wa kwanza na kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa wanyama wasio safi. 16 pWatakapokuwa na umri wa mwezi mmoja, ni lazima mtawakomboa kwa bei ya ukombozi iliyowekwa, kwa shekeli tano
Shekeli tano za fedha ni sawa na gramu 55.
za fedha, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, yenye uzito wa gera ishirini.
Gera 20 ni sawa na gramu 55.


17 s“Lakini kamwe usimkomboe mzaliwa wa kwanza wa maksai, kondoo au mbuzi; hawa ni watakatifu. Nyunyizia damu yao juu ya madhabahu na uchome mafuta yao kama sadaka itolewayo kwa moto, harufu nzuri inayompendeza Bwana. 18 tNyama zao zitakuwa chakula chenu, kama ilivyokuwa kidari cha kuinuliwa na paja la mguu wa kulia. 19 uChochote kitakachotengwa kutoka sadaka takatifu ambazo Waisraeli wanamtolea Bwana, ninakupa wewe, wanao na binti zako kama fungu lenu la kawaida. Ni Agano la milele la chumvi mbele za Bwana kwako na watoto wako.”

20 v Bwana akamwambia Aroni, “Hutakuwa na urithi wowote katika nchi yao, wala hutakuwa na sehemu miongoni mwao; Mimi ni fungu lako na urithi wako miongoni mwa Waisraeli.

21 w“Ninawapa Walawi zaka yote katika Israeli kama urithi wao kuwa kama malipo kwa kazi wanayoifanya wakati wanapohudumu katika Hema la Kukutania. 22 xKuanzia sasa, kamwe Waisraeli wasisogelee karibu na Hema la Kukutania, la sivyo watabeba matokeo ya dhambi zao, nao watakufa. 23 yNi Walawi watakaofanya kazi katika Hema la Kukutania na kubeba wajibu wa makosa dhidi yake. Hili ni agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. Hawatapokea urithi wowote miongoni mwa Waisraeli. 24 zBadala yake, ninawapa Walawi zaka zote zinazotolewa na Waisraeli kama sadaka kwa Bwana kuwa urithi wao. Hiyo ndiyo sababu nimesema hivi kuhusu wao: ‘Hawatakuwa na urithi miongoni mwa Waisraeli.’ ”

25 Bwana akamwambia Mose, 26 aa“Sema na Walawi na uwaambie: ‘Mtakapopokea zaka kutoka kwa Waisraeli ambayo ninawapa kama urithi wenu kutoka kwao, ni lazima mtoe sehemu ya kumi ya hiyo zaka kama sadaka kwa Bwana, iwe zaka ya hiyo zaka. 27 abSadaka yenu itahesabiwa kwenu kama nafaka kutoka sakafu ya kupuria, au divai kutoka kwenye shinikizo la kukamulia zabibu. 28 acKwa njia hii, ninyi pia mtatoa sadaka kwa Bwana kutoka zaka zote mtakazopokea kutoka kwa Waisraeli. Kutoka kwenye zaka hizi, ni lazima mtoe sehemu ya Bwana kwa Aroni, kuhani. 29Ni lazima mtoe kama sehemu ya Bwana iliyo nzuri sana tena ile sehemu iliyo takatifu sana kuliko zote ya kile kitu mlichopewa.’

30“Waambie Walawi: ‘Mtakapotoa sehemu zilizo bora sana, itahesabiwa kwenu kama mazao ya sakafu ya kupuria nafaka, au ya shinikizo la kukamulia zabibu. 31Ninyi na watu wa nyumbani mwenu mnaweza kula sehemu iliyobaki mahali popote, kwani ndio ujira wenu kwa ajili ya kazi yenu katika Hema la Kukutania. 32 adKwa kutoa sehemu zake zilizo bora sana, hamtakuwa na hatia katika jambo hili; ndipo hamtatia unajisi sadaka takatifu za Waisraeli, nanyi hamtakufa.’ ”

Copyright information for SwhNEN