‏ Numbers 13

Kupeleleza Kanaani

(Kumbukumbu 1:19-33)

1 Bwana akamwambia Mose, 2 a“Watume baadhi ya watu wakaipeleleze nchi ya Kanaani, ambayo ninawapa Waisraeli. Kutoka kwa kila kabila la baba zao, tuma mmoja wa viongozi wao.”

3 bHivyo kwa agizo la Bwana Mose akawatuma kutoka Jangwa la Parani. Wote walikuwa viongozi wa Waisraeli. 4Haya ndiyo majina yao:

kutoka kabila la Reubeni, Shamua mwana wa Zakuri;
5kutoka kabila la Simeoni, Shafati mwana wa Hori;
6 ckutoka kabila la Yuda, Kalebu mwana wa Yefune;
7kutoka kabila la Isakari, Igali mwana wa Yosefu;
8 dkutoka kabila la Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni;
9kutoka kabila la Benyamini, Palti mwana wa Rafu;
10kutoka kabila la Zabuloni, Gadieli mwana wa Sodi,
11kutoka kabila la Manase (kabila la Yosefu), Gadi mwana wa Susi;
12kutoka kabila la Dani, Amieli mwana wa Gemali;
13kutoka kabila la Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli;
14kutoka kabila la Naftali, Nabi mwana wa Wofsi;
15kutoka kabila la Gadi, Geueli mwana wa Maki.

16 eHaya ndiyo majina ya watu ambao Mose aliwatuma kuipeleleza nchi. (Mose akampa Hoshea mwana wa Nuni jina Yoshua.)

17 fMose alipowatuma wakaipeleleze Kanaani, alisema, “Pandeni kupitia Negebu, mwende mpaka nchi ya vilima. 18Mwone nchi ni ya namna gani, na kama watu waishio humo wana nguvu au ni wadhaifu, iwapo ni wachache au wengi. 19Wanaishi katika nchi ya namna gani? Je, ni nzuri au mbaya? Wanaishi katika miji ya namna gani? Je, haina kuta au ngome? 20 gArdhi iko aje? Ina rutuba au la? Je, kuna miti ndani yake au la? Jitahidini kadiri mwezavyo kuleta baadhi ya matunda ya nchi.” (Ulikuwa msimu wa kuiva zabibu za kwanza.)

21 hHivyo wakapanda na kuipeleleza nchi kutoka Jangwa la Sini hadi Rehobu, kuelekea Lebo-Hamathi. 22 iWakapanda kupitia Negebu hadi wakafika Hebroni, mahali ambapo Ahimani, Sheshai na Talmai, wazao wa Anaki, waliishi. (Hebroni ulikuwa umejengwa miaka saba kabla ya mji wa Soani ulioko Misri.) 23 jWalipofika katika Bonde la Eshkoli, walivunja tawi lililokuwa na kishada kimoja cha zabibu. Wawili wao wakalichukua lile tawi kwenye mti, pamoja na komamanga na tini. 24Eneo lile likaitwa Bonde la Eshkoli kwa sababu ya kile kishada cha zabibu ambacho Waisraeli walikikata huko. 25 kMwishoni mwa siku arobaini wakarudi kutoka kuipeleleza nchi.

Taarifa Juu Ya Upelelezi

26 lWakarudi kwa Mose, Aroni na jumuiya yote ya Waisraeli huko Kadeshi kwenye Jangwa la Parani. Hapo ndipo walipotoa habari kwao na kwa kusanyiko lote na kuwaonyesha matunda ya hiyo nchi. 27 mWakampa Mose taarifa hii: “Tuliingia katika nchi uliyotutuma, nayo inatiririka maziwa na asali! Hili hapa tunda lake. 28 nLakini watu wanaoishi huko ni wenye nguvu, na miji yao ina ngome na ni mikubwa sana. Huko tuliona hata wazao wa Anaki. 29 oWaamaleki wanaishi Negebu; Wahiti, Wayebusi na Waamori wanaishi katika nchi ya vilima; nao Wakanaani wanaishi karibu na bahari na kando ya Yordani.”

30 pKisha Kalebu akawanyamazisha watu mbele ya Mose na kusema, “Imetupasa kupanda na kuimiliki nchi, kwa maana hakika tunaweza kufanya hivyo.”

31 qLakini watu waliokuwa wamepanda pamoja naye wakasema, “Hatuwezi kuwashambulia wale watu; wana nguvu kutuliko sisi.” 32 rWakaeneza taarifa mbaya miongoni mwa Waisraeli kuhusu nchi waliyoipeleleza. Wakasema, “Nchi tuliyoipeleleza hula watu waishio ndani yake. Watu wote tuliowaona huko ni majitu. 33 sTuliwaona Wanefili huko (wazao wa Anaki wanatokana na Wanefili.) Tulijiona kama panzi machoni petu wenyewe, nao ndivyo walivyotuona.”

Copyright information for SwhNEN