‏ Job 9

Hotuba Ya Tatu Ya Ayubu

Hakuna Mpatanishi

1Kisha Ayubu akajibu:

2 a“Naam, najua hili ni kweli.
Lakini mwanadamu awezaje kuwa mwadilifu mbele za Mungu?
3 bIngawa mtu angetaka kushindana naye,
asingaliweza kumjibu Mungu hata mara moja miongoni mwa elfu moja.
4 cHekima yake ni kubwa sana na ana uwezo mwingi mno.
Ni nani aliyempinga naye akawa salama?
5 dAiondoa milima bila yenyewe kujua
na kuipindua kwa hasira yake.
6 eAitikisa dunia kutoka mahali pake
na kuzifanya nguzo zake zitetemeke.
7 fHusema na jua, nalo likaacha kuangaza;
naye huizima mianga ya nyota.
8 gYeye peke yake huzitandaza mbingu
na kuyakanyaga mawimbi ya bahari.
9 hYeye ndiye Muumba wa nyota za Dubu,
Nyota za Dubu hapa ina maana ya kundi la nyota za kaskazini, ambazo zinaitwa kwa jina la Dubu Mkuu.
na Orioni,
Orioni ni kundi la nyota kubwa.

Kilimia,
Kilimia ni jina lililopewa nyota saba (Taurus).
na makundi ya nyota za kusini.
10 lHutenda maajabu yasiyopimika,
miujiza isiyoweza kuhesabiwa.
11 mAnapopita karibu nami, siwezi kumwona;
apitapo mbele yangu, simtambui.
12 nAnapochukua kwa ghafula, ni nani awezaye kumzuia?
Ni nani awezaye kumwambia, ‘Unafanya nini?’
13 oMungu hataizuia hasira yake;
hata jeshi kubwa la Rahabu
Rahabu hapa ina maana ya Misri kwa fumbo.
lenye nguvu
linajikunyata miguuni pake.

14 q“Ni vipi basi mimi nitaweza kubishana naye?
Nawezaje kupata maneno ya kuhojiana naye?
15 rIngawa sikuwa na hatia, sikuweza kumjibu;
ningeweza tu kumsihi Mhukumu wangu anihurumie.
16 sHata kama ningemwita kwenye shauri, naye akakubali,
siamini kama angenisikiliza.
17 tYeye angeniangamiza kwa dhoruba
na kuongeza majeraha yangu pasipo na sababu.
18 uAsingeniacha nipumue
bali angenifunika kabisa na huzuni kuu.
19 vKama ni suala la nguvu, yeye ni mwenye nguvu!
Kama ni suala la haki, ni nani awezaye kumwita mahakamani?
20 wHata kama sikuwa na hatia, kinywa changu kingenihukumu;
kama sikuwa na kosa, kingenitangaza kuwa mwenye hatia.

21 x“Ingawa mimi sina kosa,
haileti tofauti katika nafsi yangu;
nauchukia uhai wangu.
22 yHayo yote ni sawa; ndiyo sababu nasema,
‘Yeye huwaangamiza wasio na makosa pamoja na waovu.’
23 zWakati pigo liletapo kifo cha ghafula,
yeye hudhihaki kule kukata tamaa kwa yule asiye na kosa.
24 aaWakati nchi inapoangukia mikononi mwa waovu,
yeye huwafunga macho mahakimu wake.
Kama si yeye, basi ni nani?

25 ab“Siku zangu zapita mbio kuliko mkimbiaji;
zinapita upesi bila kuona furaha hata kidogo.
26 acZinapita upesi kama mashua ya mafunjo,
mfano wa tai ayashukiaye mawindo kwa ghafula.
27 adKama nikisema, ‘Nitayasahau malalamiko yangu,
nitabadili sura ya uso wangu na kutabasamu,’
28 aebado ninahofia mateso yangu yote,
kwa kuwa ninajua hutanihesabu kuwa sina hatia.
29 afKwa kuwa nimeonekana mwenye hatia,
kwa nini basi nitaabishwe bure?
30 agHata kama ningejiosha kwa sabuni
na kutakasa mikono yangu kwa magadi,
31 ahwewe ungenitupa kwenye shimo la utelezi
kiasi kwamba hata nguo zangu zingenichukia sana.

32 ai“Yeye si mwanadamu kama mimi ili niweze kumjibu,
ili kwamba tuweze kushindana naye mahakamani.
33 ajLaiti angelikuwepo mtu wa kutupatanisha kati yetu,
aweke mkono wake juu yetu sote wawili,
34 akmtu angeliiondoa fimbo ya Mungu juu yangu,
ili utisho wake usiendelee kunitia hofu.
35 alNdipo ningenena naye, bila kumwogopa,
lakini kama ilivyo kwangu sasa, sitaweza.
Copyright information for SwhNEN