‏ Jeremiah 35

Warekabi Wasifiwa

1 aHili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Bwana, wakati wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda: 2 b“Nenda kwa jamaa ya Warekabi, uwaalike waje kwenye moja ya vyumba vya pembeni vya nyumba ya Bwana, na uwape divai wanywe.”

3Basi nikaenda kumwita Yaazania mwana wa Yeremia, mwana wa Habazinia, na ndugu zake na wanawe wote, yaani jamaa nzima ya Warekabi. 4 cNikawaleta katika nyumba ya Bwana, ndani ya chumba cha wana wa Hanani mwana wa Igdalia mtu wa Mungu. Kilikuwa karibu na chumba cha maafisa, ambacho kilikuwa juu ya kile cha Maaseya mwana wa Shalumu, aliyekuwa bawabu. 5Kisha nikaweka mabakuli yaliyojaa divai na baadhi ya vikombe mbele ya watu wa jamaa ya Warekabi na kuwaambia, “Kunyweni divai.”

6 dLakini wao wakajibu, “Sisi hatunywi divai, kwa sababu baba yetu Yonadabu mwana wa Rekabu, alitupa agizo hili: ‘Ninyi wala wazao wenu kamwe msinywe divai. 7 ePia msijenge nyumba kamwe, wala kuotesha mbegu au kupanda mashamba ya mizabibu. Kamwe msiwe na kitu chochote katika hivi, lakini siku zote lazima muishi kwenye mahema. Ndipo mtakapoishi kwa muda mrefu katika nchi ambayo ninyi ni wahamiaji.’ 8 fTumetii kila kitu ambacho baba yetu Yonadabu mwana wa Rekabu alituamuru. Sisi wenyewe wala wake zetu wala wana wetu na binti zetu kamwe hatujanywa divai 9 gwala kujenga nyumba za kuishi au kuwa na mashamba ya mizabibu, mashamba au mazao. 10Tumeishi katika mahema na tumetii kikamilifu kila kitu alichotuamuru baba yetu Yonadabu. 11 hLakini wakati Nebukadneza mfalme wa Babeli alipoivamia nchi hii, tulisema, ‘Njooni, lazima twende Yerusalemu ili kukimbia majeshi ya Wakaldayo na ya Washamu.’ Kwa hiyo tumeishi Yerusalemu.”

12Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia kusema: 13 i“Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, aliye Mungu wa Israeli, asemalo: Nenda ukawaambie watu wa Yuda na watu wa Yerusalemu, ‘Je, hamwezi kujifunza kutoka kwa wana wa Rekabu, na kuyatii maneno yangu?’ asema Bwana. 14 j‘Yonadabu mwana wa Rekabu aliwaagiza wanawe wasinywe divai, na agizo hilo wamelishika mpaka leo hawanywi divai, kwa sababu wanatii amri ya baba yao. Lakini nimenena nanyi tena na tena, lakini hamkunitii mimi. 15 kTena na tena nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu. Wakasema, “Kila mmoja wenu ni lazima ageuke na kuacha njia zake mbaya, na kuyatengeneza matendo yake. Msifuate miungu mingine ili kuitumikia. Ndipo mtakapoishi katika nchi niliyowapa ninyi na baba zenu.” Lakini hamkujali wala kunisikiliza. 16 lWazao wa Yonadabu mwana wa Rekabu walitimiza amri ambayo baba yao aliwapa, lakini watu hawa hawakunitii mimi.’

17 m“Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Sikilizeni! Nitaleta juu ya Yuda na juu ya kila mmoja aishiye Yerusalemu kila aina ya maafa niliyotamka dhidi yao. Nilinena nao, lakini hawakusikiliza. Niliwaita, lakini hawakujibu.’ ”

18 nKisha Yeremia akaiambia jamaa ya Warekabi, “Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: ‘Mmetii amri ya baba yenu Yonadabu, na mmefuata mafundisho yake yote na mmefanya kila kitu alichowaamuru.’ 19 oKwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Yonadabu mwana wa Rekabu hatakosa kamwe kuwa na mtu wa kunitumikia mimi.’ ”

Copyright information for SwhNEN