‏ Jeremiah 12

Lalamiko La Yeremia

1 aWewe daima u mwenye haki, Ee Bwana,
niletapo mashtaka mbele yako.
Hata hivyo nitazungumza nawe kuhusu hukumu yako:
Kwa nini njia ya waovu inafanikiwa?
Kwa nini wasio waaminifu
wote wanaishi kwa raha?
2 bUmewapanda, nao wameota,
wanakua na kuzaa matunda.
Daima u midomoni mwao,
lakini mbali na mioyo yao.
3 cHata hivyo unanijua mimi, Ee Bwana;
unaniona na kuyachunguza mawazo yangu kukuhusu wewe.
Wakokote kama kondoo wanaokwenda kuchinjwa!
Watenge kwa ajili ya siku ya kuchinjwa!
4 dJe, nchi itakaa katika hali ya kuomboleza mpaka lini,
na majani katika kila shamba kunyauka?
Kwa sababu wale waishio ndani yake ni waovu,
wanyama na ndege wameangamia.
Zaidi ya hayo, watu wanasema,
Bwana hataona yatakayotupata sisi.”

Jibu La Mungu

5 e“Ikiwa umeshindana mbio na watu kwa mguu na wakakushinda,
unawezaje kushindana na farasi?
Ikiwa unajikwaa kwenye nchi ambayo ni salama,
utawezaje kwenye vichaka kando ya Yordani?
6 fNdugu zako, watu wa jamaa yako mwenyewe:
hata wao wamekusaliti;
wameinua kilio kikubwa dhidi yako.
Usiwaamini, ingawa wanazungumza
mema juu yako.

7“Nitaiacha nyumba yangu,
nitupe urithi wangu;
nitamtia yeye nimpendaye
mikononi mwa adui zake.
8 gUrithi wangu umekuwa kwangu
kama simba wa msituni.
Huningurumia mimi,
kwa hiyo ninamchukia.
9 hJe, urithi wangu haukuwa
kama ndege wa mawindo wa madoadoa
ambaye ndege wengine wawindao
humzunguka na kumshambulia?
Nenda ukawakusanye pamoja wanyama wote wa mwituni;
walete ili wale.
10 iWachungaji wengi wataliharibu shamba langu la mizabibu
na kulikanyaga shamba langu;
watalifanya shamba langu zuri
kuwa jangwa la ukiwa.
11 jLitafanywa kuwa jangwa,
lililokauka na kuachwa ukiwa mbele zangu;
nchi yote itafanywa jangwa
kwa sababu hakuna hata mmoja anayejali.
12 kJuu ya miinuko yote ilivyo kama jangwani
mharabu atajaa,
kwa maana upanga wa Bwana utawala,
kuanzia ncha moja ya nchi hadi nyingine;
hakuna hata mmoja atakayekuwa salama.
13 lWatapanda ngano lakini watavuna miiba;
watajitaabisha lakini hawatafaidi chochote.
Kwa hiyo beba aibu ya mavuno yako
kwa sababu ya hasira kali ya Bwana Mungu.”
14 mHili ndilo asemalo Bwana: “Kwa habari ya majirani zangu wote wabaya wanaonyangʼanya urithi ambao ninawapa watu wangu Israeli, nitawangʼoa kutoka nchi zao, nami nitaingʼoa nyumba ya Yuda kutoka katikati yao. 15 nLakini baada ya kuwangʼoa, nitawahurumia tena na kumrudisha kila mmoja wao kwenye urithi wake mwenyewe na kwenye nchi yake mwenyewe. 16 oIkiwa watajifunza vyema njia za watu wangu na kuapa kwa Jina langu, wakisema, ‘Hakika kama Bwana aishivyo,’ hata kama wakati fulani walifundisha watu wangu kuapa kwa Baali, ndipo watakapofanywa imara katikati ya watu wangu. 17 pLakini kama taifa lolote halitasikiliza na kutii, nitalingʼoa kabisa na kuliangamiza,” asema Bwana.

Copyright information for SwhNEN