‏ Isaiah 44

Israeli Aliyechaguliwa

1 a“Lakini sasa sikiliza, ee Yakobo, mtumishi wangu,
Israeli, niliyemchagua.
2 bHili ndilo asemalo Bwana,
yeye aliyekuhuluku, aliyekuumba tumboni,
yeye atakayekusaidia:
Usiogope, ee Yakobo, mtumishi wangu,
Yeshuruni,
Yeshuruni hapa maana yake ni Yeye aliye mnyofu, yaani Israeli (ona pia Kum 32:15).
niliyekuchagua.
3 dKwa maana nitamimina maji juu ya nchi yenye kiu,
na vijito vya maji juu ya ardhi iliyokauka;
nitamimina Roho wangu juu ya watoto wako,
nayo baraka yangu juu ya wazao wako.
4 eNao watachipua kama manyasi katika shamba la majani,
kama mierezi kando ya vijito vya maji yatiririkayo.
5 fMmoja atasema, ‘Mimi ni wa Bwana’;
mwingine atajiita kwa jina la Yakobo;
vilevile mwingine ataandika juu ya mkono wake, ‘Wa Bwana,’
na kujiita kwa jina la Israeli.

Ni Bwana, Siyo Sanamu

6 g“Hili ndilo asemalo Bwana,
Mfalme wa Israeli na Mkombozi,
Bwana Mwenye Nguvu Zote:
Mimi ni wa kwanza na Mimi ni wa mwisho;
zaidi yangu hakuna Mungu.
7 hNi nani basi aliye kama mimi? Yeye na atangaze.
Yeye atangaze na kuweka mbele yangu
ni kitu gani kilichotokea tangu nilipoumba watu wangu wa kale,
tena ni nini kitakachotokea:
naam, yeye na atoe unabii ni nini kitakachokuja.
8 iMsitetemeke, msiogope.
Je, sikutangaza hili, na kutoa unabii tangu zamani?
Ninyi ni mashahidi wangu.
Je, yuko Mungu zaidi yangu mimi?
Hasha, hakuna Mwamba mwingine;
mimi simjui mwingine.”

9 jWote wachongao sanamu ni ubatili,
navyo vitu wanavyovithamini havifai kitu.
Wale ambao wanazitetea ni vipofu,
ni wajinga, nao waaibika.
10 kNi nani atengenezaye mungu na kusubu sanamu,
ambayo haiwezi kumfaidia kitu chochote?
11 lYeye pamoja na wenziwe wa aina yake wataaibishwa,
mafundi wao si kitu ila ni wanadamu tu.
Wote wakusanyike pamoja na kuwa na msimamo wao,
watashushwa chini kwa hofu na kwa fedheha.

12 mMuhunzi huchukua kifaa
na kukifanyia kazi kwenye makaa ya moto,
hutengeneza sanamu kwa nyundo,
huifanyiza kwa nguvu za mkono wake.
Huona njaa na kupoteza nguvu zake,
asipokunywa maji huzimia.
13 nSeremala hupima kwa kutumia kamba
na huuchora mstari kwa kalamu;
huchonga kwa patasi
na kutia alama kwa bikari.
Huifanyiza katika umbo la binadamu,
la mwanadamu katika utukufu wake wote,
ili iweze kukaa katika sehemu yake ya ibada ya miungu.
14 oHukata miti ya mierezi,
huchukua mtiriza au mwaloni.
Huuacha ukue miongoni mwa miti ya msituni,
au hupanda msunobari, nayo mvua huufanya ukue.
15 pNi kuni ya binadamu:
yeye huchukua baadhi yake na kuota moto,
huwasha moto na kuoka mkate.
Lakini pia huutumia kumtengeneza mungu na akamwabudu,
huitengeneza sanamu na kuisujudia.
16 qSehemu ya kuni huziweka motoni,
akapikia chakula chake,
hubanika nyama na kula hadi ashibe.
Huota moto na kusema,
“Aha! Ninahisi joto, ninaona moto.”
17 rMabaki yake hutengeneza mungu, sanamu yake;
yeye huisujudia na kuiabudu.
Huiomba na kusema,
“Niokoe; wewe ni mungu wangu.”
18 sHawajui chochote, hawaelewi chochote,
macho yao yamefungwa hata hawawezi kuona,
akili zao zimefungwa hata hawawezi kufahamu.
19 tHakuna anayefikiri,
hakuna mwenye maarifa wala ufahamu wa kusema,
“Sehemu yake nilitumia kwa kuni;
hata pia nilioka mkate juu ya makaa yake,
nikabanika nyama na kuila.
Je, nifanye machukizo kwa kile kilichobaki?
Je, nisujudie gogo la mti?”
20 uHujilisha kwa majivu, moyo uliodanganyika humpotosha;
hawezi kujiokoa mwenyewe, au kusema,
“Je, kitu hiki kilichoko katika mkono wangu wa kuume si ni uongo?”

21 v“Ee Yakobo, kumbuka mambo haya,
ee Israeli, kwa kuwa wewe ni mtumishi wangu.
Nimekuumba wewe, wewe ni mtumishi wangu.
Ee Israeli, sitakusahau.
22 wNimeyafuta makosa yako kama wingu,
dhambi zako kama ukungu wa asubuhi.
Nirudie mimi,
kwa kuwa nimekukomboa wewe.”

23 xEnyi mbingu, imbeni kwa furaha,
kwa maana Bwana amefanya jambo hili.
Ee vilindi vya dunia, piga kelele.
Enyi milima, pazeni sauti kwa nyimbo,
enyi misitu na miti yenu yote,
kwa maana Bwana amemkomboa Yakobo,
ameuonyesha utukufu wake katika Israeli.

Yerusalemu Kukaliwa

24 y“Hili ndilo asemalo Bwana,
Mkombozi wako, aliyekuumba tumboni:

“Mimi ni Bwana,
niliyeumba vitu vyote,
niliyezitanda mbingu peke yangu,
niliyeitandaza nchi mwenyewe,

25 z“mimi huzipinga ishara za manabii wa uongo,
na kuwatia upumbavu waaguzi,
niyapinduaye maarifa ya wenye hekima,
na kuyafanya kuwa upuzi,
26 aaniyathibitishaye maneno ya watumishi wake,
na kutimiza utabiri wa wajumbe wake,

“niambiaye Yerusalemu, ‘Itakaliwa na watu,’
niambiaye miji ya Yuda kuwa, ‘Itajengwa,’
na kuhusu magofu yake, ‘Mimi nitayatengeneza,’
27 abniambiaye kilindi cha maji, ‘Kauka,
nami nitakausha vijito vyako,’
28 acnisemaye kuhusu Koreshi, ‘Yeye ni mchungaji wangu,
naye atatimiza yote yanipendezayo;
atauambia Yerusalemu, “Ukajengwe tena,”
na kuhusu Hekalu, “Misingi yake na iwekwe.” ’
Copyright information for SwhNEN