‏ Isaiah 43

Mwokozi Pekee Wa Israeli

1 aLakini sasa hili ndilo asemalo Bwana,
yeye aliyekuumba, ee Yakobo,
yeye aliyekuhuluku, ee Israeli:
“Usiogope kwa maana nimekukomboa,
nimekuita wewe kwa jina lako, wewe u wangu.
2 bUnapopita kwenye maji makuu,
nitakuwa pamoja nawe,
unapopita katika mito ya maji,
hayatakugharikisha.
Utakapopita katika moto,
hutaungua,
miali ya moto haitakuunguza.
3 cKwa kuwa Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako.
Ninaitoa Misri kuwa fidia yako,
Kushi na Seba badala yako.
4 dKwa kuwa wewe ni wa thamani na wa kuheshimiwa machoni pangu,
nami kwa kuwa ninakupenda,
nitatoa watu badala yako
na mataifa badala ya maisha yako.
5 eUsiogope, kwa kuwa mimi nipo pamoja nawe,
nitawaleta watoto wako kutoka mashariki,
na kukukusanya kutoka magharibi.
6 fNitaiambia kaskazini, ‘Watoe!’
nayo kusini, ‘Usiwazuie.’
Walete wana wangu kutoka mbali,
na binti zangu kutoka miisho ya dunia:
7 gkila mmoja ambaye ameitwa kwa Jina langu,
niliyemuumba kwa utukufu wangu,
niliyemhuluku na kumfanya.”
8 hUwaongoze wale wenye macho lakini hawaoni,
wenye masikio lakini hawasikii.
9 iMataifa yote yanakutanika pamoja,
na makabila yanakusanyika.
Ni nani miongoni mwao aliyetangulia kutuambia haya,
na kututangazia mambo yaliyopita?
Walete mashahidi wao ili kuwathibitisha kuwa walikuwa sahihi,
ili wengine waweze kusikia, waseme, “Ni kweli.”

10 j“Ninyi ni mashahidi wangu,” asema Bwana,
“na mtumishi wangu niliyemchagua,
ili mpate kunijua na kuniamini,
na kutambua kwamba Mimi ndiye.
Kabla yangu hakuna mungu aliyefanyizwa,
wala hatakuwepo mwingine baada yangu.
11 kMimi, naam mimi, ndimi Bwana,
zaidi yangu hakuna mwokozi.
12 lNimedhihirisha, kuokoa na kutangaza:
Mimi, wala si mungu mgeni katikati yenu.
Ninyi ni mashahidi wangu,” asema Bwana,
“kwamba Mimi ndimi Mungu.
13 mNaam, tangu siku za kale, Mimi ndiye.
Hakuna hata mmoja awezaye kuokoa
kutoka mkononi wangu.
Mimi ninapotenda,
ni nani awezaye kutangua?”

Huruma Za Mungu, Na Kukosa Uaminifu Kwa Israeli

14 nHili ndilo Bwana asemalo,
Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli:
“Kwa ajili yenu nitatumana Babeli
na kuwaleta Wakaldayo wote kama wakimbizi,
katika meli walizozionea fahari.
15 oMimi ndimi Bwana, yeye Aliye Mtakatifu wako,
Muumba wa Israeli, Mfalme wako.”

16 pHili ndilo asemalo Bwana,
yeye aliyefanya njia baharini,
mahali pa kupita kwenye maji mengi,
17 qaliyeyakokota magari ya vita na farasi,
jeshi pamoja na askari wa msaada,
nao wakalala huko, wala hawatainuka tena kamwe,
wakakomeshwa, na wakazimika kama utambi:
18 r“Msiyakumbuke mambo yaliyopita,
wala msiyatafakari mambo ya zamani.
19 sTazama, nitafanya jambo jipya!
Sasa litachipuka, je, hamtalitambua?
Nitafanya njia jangwani
na vijito vya maji katika nchi kame.
20 tWanyama wa mwituni wataniheshimu,
mbweha na bundi,
kwa sababu ninawapatia maji jangwani,
na vijito katika nchi kame,
ili kuwapa watu wangu maji, wale niliowachagua,
21 uwatu wale niliowaumba kwa ajili yangu,
ili wapate kutangaza sifa zangu.

22“Hata hivyo hukuniita mimi, ee Yakobo,
hujajitaabisha kwa ajili yangu, ee Israeli.
23 vHujaniletea kondoo kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa,
wala kuniheshimu kwa dhabihu zako.
Sikukulemea kwa sadaka za nafaka
wala kukuchosha kwa kuhitaji uvumba.
24 wHukuninunulia uvumba wowote wenye manukato,
wala hukunipa kwa ukarimu
mafuta ya wanyama wa dhabihu zako.
Lakini umenilemea kwa dhambi zako,
na kunitaabisha kwa makosa yako.

25 x“Mimi, naam mimi, ndimi nizifutaye dhambi zako,
kwa ajili yangu mwenyewe,
wala sizikumbuki dhambi zako tena.
26 yTafakari mambo yaliyopita,
njoo na tuhojiane,
leta shauri lako uweze kupewa haki yako.
27 zBaba yako wa kwanza alitenda dhambi,
wasemaji wako wameasi dhidi yangu.
28 aaKwa hiyo nitawaaibisha wakuu wa Hekalu lako,
nami nitamtoa Yakobo aangamizwe,
na Israeli adhihakiwe.
Copyright information for SwhNEN