‏ Isaiah 21

Unabii Dhidi Ya Babeli

1Neno kuhusu Jangwa kando ya Bahari:
Kama upepo wa kisulisuli unaopita katika nchi hadi kusini,
mshambuliaji anakuja kutoka jangwani,
kutoka nchi inayotisha.

2 aNimeonyeshwa maono ya kutisha:
Msaliti anasaliti, mteka nyara anateka nyara.
Elamu, shambulia! Umedi, izunguke kwa jeshi!
Nitakomesha huzuni zote alizosababisha.

3 bKatika hili mwili wangu umeteswa na maumivu,
maumivu makali ya ghafula yamenishika,
kama yale ya mwanamke mwenye utungu wa kuzaa.
Nimeduwazwa na lile ninalolisikia,
nimeshangazwa na lile ninaloliona.
4 cMoyo wangu unababaika,
woga unanifanya nitetemeke,
gizagiza la jioni nililolitamani sana,
limekuwa hofu kuu kwangu.

5 dWanaandaa meza,
wanatandaza mazulia,
wanakula, wanakunywa!
Amkeni, enyi maafisa,
zitieni ngao mafuta!
6 eHili ndilo Bwana analoniambia:

“Nenda, weka mlinzi,
na atoe taarifa ya kile anachokiona.
7 fAnapoona magari ya vita
pamoja na kundi la farasi,
wapanda punda au wapanda ngamia,
na awe macho, awe macho kikamilifu.”
8 gNaye mlinzi alipaza sauti,

“Mchana baada ya mchana, bwana wangu, ninasimama katika mnara wa ulinzi,
kila usiku ninakaa mahali pangu nilipoamriwa.
9 hTazama, yuaja mtu anayepanda gari la vita
pamoja na kundi la farasi.
Naye anajibu:
‘Babeli umeanguka, umeanguka!
Vinyago vyote vya miungu yake
vimelala chini vikiwa vimevunjwa!’ ”

10 iEe watu wangu, mliopondwa kwenye sakafu ya kupuria,
ninawaambia kile nilichokisikia
kutoka kwa Bwana Mwenye Nguvu Zote,
kutoka kwa Mungu wa Israeli.

Unabii Dhidi Ya Edomu

11 jNeno kuhusu Duma:

Mtu fulani ananiita kutoka Seiri,
“Mlinzi, usiku utaisha lini?
Mlinzi, usiku utaisha lini?”
12Mlinzi anajibu,
“Asubuhi inakuja, lakini pia usiku.
Kama ungeliuliza, basi uliza;
bado na urudi tena.”

Unabii Dhidi Ya Arabia

13 kNeno kuhusu Arabia:

Enyi misafara ya Wadedani,
mnaopiga kambi katika vichaka vya Arabia,
14 lleteni maji kwa wenye kiu,
ninyi mnaoishi Tema,
leteni chakula kwa ajili ya wakimbizi.
15 mWanaukimbia upanga,
kutoka upanga uliochomolewa alani,
kutoka upinde uliopindwa,
na kutoka kwenye joto la vita.
16 nHili ndilo Bwana analoniambia: “Katika muda wa mwaka mmoja, kama vile mtumishi aliyefungwa na mkataba angeihesabu, majivuno yote ya Kedari yatafikia mwisho. 17 oWanaume wavutao pinde walionusurika, mashujaa wa Kedari, watakuwa wachache.” Bwana, Mungu wa Israeli, amesema.

Copyright information for SwhNEN