‏ Habakkuk 2

1 aNitasimama katika zamu yangu,
na kujiweka mwenyewe juu ya maboma;
nitatazama nione atakaloniambia,
na ni jibu gani nitakalotoa kuhusu lalamiko hili.

Jibu La Bwana

2 bKisha Bwana akajibu:

“Andika ufunuo huu,
na ukaufanye wazi juu ya vibao,
ili mpiga mbiu akimbie nao.
3 cKwa kuwa ufunuo huu unasubiri wakati uliokubalika;
unazungumzia mambo ya mwisho,
na kamwe hautakosea.
Iwapo utakawia, wewe usubiri;
kwa hakika utakuja na hautachelewa.

4 d“Tazama, amejaa majivuno;
anavyovitamani si vya unyofu:
lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake:
5 ehakika mvinyo humsaliti;
ni mwenye kiburi na hana amani.
Kwa sababu ni mlafi kama kuzimu
na kama kifo kamwe hatosheki;
anajikusanyia mataifa yote
na kuchukua watu wote mateka.
6 f“Je, watu wote hawatamsuta kwa dhihaka na kumbeza, wakisema,

“ ‘Ole wake yeye akusanyaye bidhaa zilizoibwa
na kujifanyia utajiri kwa kutoza kwa nguvu!
Ataendelea hivi kwa muda gani?’
7 gJe, wadai wako hawatainuka ghafula?
Je, hawataamka na kukufanya utetemeke?
Kisha utakuwa mhanga kwao.
8 h iKwa kuwa umeteka nyara mataifa mengi,
watu waliobaki watakuteka nyara wewe.
Kwa kuwa umemwaga damu ya mtu;
umeharibu nchi na miji, na kila mmoja ndani yake.

9 j“Ole wake yeye ajengaye milki yake kwa mapato ya udhalimu,
awekaye kiota chake juu,
ili kukimbia makucha ya uharibifu!
10 kUmefanya shauri la maangamizi ya watu wengi,
ukiaibisha nyumba yako mwenyewe, na kupotewa na maisha yako.
11 lMawe ya kuta yatapiga kelele,
na mihimili ya kazi ya mbao itarudisha mwangwi wake.

12 m“Ole wake yeye ajengaye mji kwa kumwaga
damu na kuusimamisha mji kwa uhalifu!
13 nJe, Bwana Mwenye Nguvu Zote hakuonyesha
kwamba kazi ya wanadamu ni mafuta tu kwa ajili ya moto,
na kwamba mataifa
yanajichosha bure?
14 oKwa kuwa dunia itajazwa na maarifa ya utukufu wa Bwana,
kama maji yaifunikavyo bahari.

15 p“Ole wake yeye awapaye jirani zake kileo,
akiimimina kutoka kwenye kiriba
cha mvinyo mpaka wamelewa,
ili apate kutazama miili yao iliyo uchi.
16 qUtajazwa na aibu badala ya utukufu.
Sasa ni zamu yako! Kunywa na ujifunue!
Kikombe kutoka kwenye mkono wa kuume wa Bwana kinakujia,
na aibu itafunika utukufu wako.
17 rUkatili ulioifanyia Lebanoni utakufunika,
na uharibifu uliowafanyia wanyama utakutisha.
Kwa sababu umemwaga damu ya mtu;
umeharibu nchi na miji na kila mmoja aliyeko ndani yake.

18 s“Sanamu ina thamani gani,
kwani mwanadamu ndiye alichonga?
Ama kinyago kinachofundisha uongo?
Kwa kuwa yeye aliyekitengeneza
hutegemea kazi ya mikono yake mwenyewe;
hutengeneza sanamu zisizoweza kuzungumza.
19 tOle wake yeye auambiaye mti, ‘Uwe hai!’
Ama asemaye na jiwe lisilo na uhai, ‘Amka!’
Je, linaweza kuongoza?
Limefunikwa kwa dhahabu na fedha;
hakuna pumzi ndani yake.
20 uLakini Bwana yuko katika Hekalu lake takatifu;
dunia yote na inyamaze mbele yake.”
Copyright information for SwhNEN