Ezekiel 29
Unabii Dhidi Ya Misri
1Katika mwaka wa kumi, mwezi wa kumi, siku ya kumi na mbili, neno la Bwana likanijia kusema: 2 a“Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Farao mfalme wa Misri na utabiri dhidi yake na dhidi ya Misri yote. 3 bNena, nawe useme: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:“ ‘Mimi ni kinyume nawe, Farao, mfalme wa Misri,
joka kubwa ulalaye katikati ya vijito vyako.
Unasema, “Mto Naili ni wangu mwenyewe;
niliufanya kwa ajili yangu mwenyewe.”
4 cLakini nitatia ndoana katika mataya yako
nami nitawafanya samaki wa vijito vyako
washikamane na magamba yako.
Nitakutoa katikati ya vijito vyako,
pamoja na samaki wote
walioshikamana na magamba yako.
5 dNitakutupa jangwani,
wewe pamoja na samaki wote wa vijito vyako.
Utaanguka uwanjani,
nawe hutakusanywa au kuchukuliwa.
Nitakutoa uwe chakula
kwa wanyama wa nchi
na ndege wa angani.
6 eNdipo wale wote waishio Misri watakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.
“ ‘Umekuwa fimbo ya tete kwa nyumba ya Israeli. 7 fWalipokushika kwa mikono yao, ulivunjika na kuchana mabega yao; walipokuegemea, ulivunjika na migongo yao ikateguka.
8 g“ ‘Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitaleta upanga juu yako na kuua watu wako na wanyama wao. 9 hMisri itakuwa ukiwa na isiyolimwa wala kukaliwa na watu. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.
“ ‘Kwa sababu ulisema, “Mto Naili ni wangu; mimi niliufanya,” 10 ikwa hiyo mimi ni kinyume nawe na kinyume na vijito vyako, nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa magofu na ukiwa isiyolimwa wala kukaliwa na watu kuanzia Migdoli hadi Aswani, hata kufikia mpakani wa Ethiopia. 11 jHakuna unyayo wa mtu au mnyama utakaopita ndani yake, wala hakuna yeyote atakayeishi humo kwa muda wa miaka arobaini. 12 kNitaifanya nchi ya Misri ukiwa, miongoni mwa nchi zilizo ukiwa, nayo miji yake itabaki ukiwa miaka arobaini miongoni mwa miji iliyo magofu. Nami nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwafukuza huku na huko katika nchi nyingine.
13 l“ ‘Lakini hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Mwishoni mwa hiyo miaka arobaini, nitawakusanya Wamisri kutoka mataifa walikotawanywa. 14 mNitawarudisha hao Wamisri kutoka kwenye kutekwa kwao na kuwaweka katika Pathrosi, ▼
▼Pathrosi ni Misri ya Juu.
nchi ya baba zao. Huko watakuwa na ufalme usiokuwa na nguvu. 15 oUtakuwa ufalme dhaifu kuliko zote na kamwe Misri haitajikweza tena juu ya mataifa mengine. Nitaufanya ufalme wake dhaifu sana kiasi kwamba kamwe hautatawala tena juu ya mataifa mengine. 16 pMisri haitakuwa tena tumaini la watu wa Israeli bali itakuwa kumbukumbu ya dhambi yao kwa kuigeukia kuomba msaada. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana Mwenyezi.’ ” 17 qKatika mwaka wa ishirini na saba, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza, neno la Bwana likanijia, kusema: 18 r“Mwanadamu, Nebukadneza mfalme wa Babeli aliongoza jeshi lake kufanya kazi ngumu dhidi ya Tiro; kila kichwa kilipata upaa na kila bega likachunika. Lakini yeye na jeshi lake hawakupata malipo yoyote kutokana na muda wote aliongoza hiyo vita dhidi ya Tiro. 19 sKwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitaitia Misri mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, naye atachukua utajiri wa Misri. Atateka mateka na kuchukua nyara mali za Misri kama ujira kwa ajili ya jeshi lake. 20 tNimempa mfalme wa Babeli nchi ya Misri kuwa ujira kwa juhudi zake kwa sababu yeye na jeshi lake walifanya kwa ajili yangu, asema Bwana Mwenyezi.
21 u“Katika siku hiyo nitaifanya nyumba ya Israeli iwe na nguvu nami nitakifungua kinywa chako miongoni mwao. Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana.”
Copyright information for
SwhNEN