‏ Deuteronomy 6

Mpende Bwana Mungu Wako

1Haya ndiyo maagizo, amri na sheria ambazo Bwana Mungu wenu aliniagiza niwafundishe ninyi ili mpate kuyashika katika nchi ambayo ninyi mnavuka Yordani kuimiliki, 2 aili kwamba ninyi, watoto wenu na watoto wao baada yao wamche Bwana Mungu wenu siku zote kwa kushika amri na maagizo yake yote ninayowapa, ili mweze kuyafurahia maisha marefu. 3 bSikia, ee Israeli, nawe uwe mwangalifu kutii ili upate kufanikiwa na kuongezeka sana katika nchi itiririkayo maziwa na asali, kama Bwana, Mungu wa baba zenu, alivyowaahidi ninyi.

4 cSikia, ee Israeli: Bwana Mungu wako, Bwana ni mmoja. 5 dMpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. 6 eAmri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. 7 fWafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo. 8 gZifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako. 9 hZiandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako.

10 iWakati Bwana Mungu wako atakapokuleta katika nchi aliyowaapia baba zako, Abrahamu, Isaki na Yakobo, kukupa wewe, nchi kubwa, ina miji inayopendeza ambayo hukuijenga, 11 jnyumba zilizojaa vitu vizuri vya aina nyingi ambavyo hukuvijaza, visima ambavyo hukuchimba, na mashamba ya mizabibu na mizeituni ambayo hukupanda wewe, basi, utakapokula na kushiba, 12 kjihadhari usije ukamwacha Bwana, aliyekutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa.

13 lUtamcha Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake na kuapa kwa jina lake. 14Usifuate miungu mingine, miungu ya mataifa yanayokuzunguka; 15 mkwa kuwa Bwana Mungu wako, ambaye yuko katikati yako, ni Mungu mwenye wivu na hasira yake itawaka dhidi yako, naye atakuangamiza kutoka uso wa nchi. 16 nUsimjaribu Bwana Mungu wako kama ulivyofanya huko Masa. 17 oUtayashika maagizo ya Bwana Mungu wako kwa bidii, na masharti na amri alizokupa. 18 pFanya lililo haki na jema mbele za Bwana, ili upate kufanikiwa, uweze kuingia na kuimiliki nchi nzuri ambayo Bwana aliahidi kwa kiapo kwa baba zako, 19 qkuwafukuza kwa nguvu adui zako mbele yako kama Bwana alivyosema.

20 rSiku zijazo, mtoto wako atakapokuuliza, “Ni nini maana ya masharti haya, amri na sheria hizi ambazo Bwana Mungu wako alikuagiza wewe?” 21 sMwambie: “Tulikuwa watumwa wa Farao huko Misri, lakini Bwana alitutoa sisi kutoka Misri kwa mkono wenye nguvu. 22Bwana akapeleka mbele yetu ishara za miujiza na maajabu makubwa na ya kutisha mno juu ya Misri na Farao pamoja na nyumba yake yote. 23Lakini Mungu akatutoa huko, akatuleta na kutupa nchi hii ambayo aliwaahidi baba zetu kwa kiapo. 24 tBwana akatuagiza tutii amri hizi zote na kumcha Bwana Mungu wetu, ili tupate kustawi na kuendelea kuwa hai kama ilivyo leo. 25 uKama tukizitii kwa bidii amri hizi zote mbele za Bwana Mungu wetu, kama alivyotuamuru sisi, hiyo itakuwa haki yetu.”

Copyright information for SwhNEN