‏ 2 Chronicles 29

Hezekia Mfalme Wa Yuda

(2 Wafalme 18:1-12)

1 aHezekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Mama yake aliitwa Abiya binti Zekaria. 2 bAkafanya yaliyo mema machoni pa Bwana kama Daudi baba yake alivyofanya.

3 cKatika mwezi wa kwanza wa mwaka wa kwanza wa utawala wa alifungua milango ya Hekalu la Bwana, na kuikarabati. 4Akawaingiza makuhani na Walawi ndani na kuwakutanisha katika uwanja upande wa mashariki 5 dna kusema: “Nisikilizeni mimi, enyi Walawi! Jitakaseni nafsi zenu sasa, mkaitakase na nyumba ya Bwana, Mungu wa baba zenu. Ondoeni uchafu wote kutoka mahali patakatifu. 6 eBaba zetu hawakuwa waaminifu, walifanya maovu machoni pa Bwana Mungu wetu na wakamwacha yeye. Wakageuza nyuso zao mbali na Maskani ya Bwana wakamgeuzia visogo vyao. 7 fPia walifunga milango ya ukumbi wa Hekalu na kuzima taa zake. Hawakufukiza uvumba wala kutoa sadaka yoyote ya kuteketezwa katika mahali patakatifu kwa Mungu wa Israeli. 8 gKwa hiyo, hasira ya Bwana ikashuka juu ya Yuda na Yerusalemu, naye akawa amewafanya kitu cha kutisha, cha kushangaza na kitu cha kufanyia mzaha kama mnavyoona kwa macho yenu wenyewe. 9 hHii ndiyo sababu baba zetu wameanguka kwa upanga na ndiyo sababu wana wetu na binti zetu, pia wake zetu wamekuwa mateka. 10 iSasa ninadhamiria moyoni mwangu kuweka Agano na Bwana, Mungu wa Israeli, ili hasira yake kali igeuziwe mbali nasi. 11 jWanangu, basi msipuuze jambo hili sasa, kwa kuwa Bwana amewachagua ninyi msimame mbele zake na kumtumikia, mkawe watumishi wake na mkamfukizie uvumba.”

12 kNdipo Walawi wafuatao wakaanza kazi:

Kutoka kwa Wakohathi,
Mahathi mwana wa Amasai na Yoeli mwana wa Azaria;
kutoka kwa Wamerari,
Kishi mwana wa Abdi na Azaria mwana wa Yahaleleli;
kutoka kwa Wagershoni,
Yoa mwana wa Zima na Edeni mwana wa Yoa;
13 lkutoka kwa wana wa Elisafani,
Shimri na Yeieli;
kutoka kwa wana wa Asafu,
Zekaria na Matania;
14kutoka kwa wana wa Hemani,
Yehieli na Shimei;
kutoka kwa wana wa Yeduthuni,
Shemaya na Uzieli.
15 mWalipomaliza kuwakusanya ndugu zao na kujiweka wakfu, wakaingia ndani ili kutakasa Hekalu la Bwana, kama vile mfalme alivyokuwa ameagiza, kwa kufuata neno la Bwana. 16 nMakuhani wakaingia patakatifu pa Hekalu la Bwana ili kupatakasa. Wakatoa nje penye ua wa Hekalu la Mungu kila kitu kichafu walichokikuta kwenye Hekalu la Bwana. Walawi wakavichukua na kuvipeleka nje katika Bonde la Kidroni. 17 oWalianza kazi ya utakaso siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza na kufikia siku ya nane ya mwezi huo wakawa wamefikia kwenye ukumbi wa Bwana. Kwa siku zingine nane wakalitakasa Hekalu lenyewe la Bwana wakakamilisha katika siku ya kumi na sita ya mwezi huo wa kwanza.

18Kisha wakaingia ndani kwa Mfalme Hezekia kutoa habari na kusema: “Tumelitakasa Hekalu lote la Bwana, madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa pamoja na vyombo vyake vyote, meza ya kupanga mikate iliyowekwa wakfu, pamoja na vyombo vyake vyote. 19 pTumeviandaa na kuvitakasa vyombo vyote vile ambavyo Mfalme Ahazi, kwa kukosa uaminifu kwake, aliviondoa wakati alipokuwa mfalme. Sasa viko mbele ya madhabahu ya Bwana.”

Ibada Hekaluni Yarejeshwa

20Ndipo Mfalme Hezekia akainuka asubuhi na mapema, akakusanya pamoja maafisa wa mji wakakwea hekaluni mwa Bwana. 21 qWakaleta mafahali saba, kondoo dume saba, wana-kondoo dume saba na mabeberu saba kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya ufalme, kwa ajili ya mahali patakatifu na kwa ajili ya Yuda. Mfalme akawaamuru makuhani, wazao wa Aroni, kuvitoa vitu hivyo sadaka katika madhabahu ya Bwana. 22 rHivyo wakachinja wale mafahali, nao makuhani wakachukua ile damu na kuinyunyiza kwenye madhabahu, halafu wakawachinja wale kondoo dume saba na kunyunyiza hiyo damu yao kwenye madhabahu, kisha wakawachinja wale wana-kondoo dume na kunyunyiza damu yao kwenye madhabahu. 23 sWale mabeberu waliokuwa kwa ajili ya sadaka ya dhambi wakaletwa mbele ya mfalme na kusanyiko nao wakaweka mikono yao juu hao mabeberu. 24 tNdipo makuhani wakawachinja hao mabeberu na kuweka damu yao kwenye madhabahu kwa ajili ya sadaka ya dhambi ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Israeli yote, kwa sababu mfalme alikuwa ameamuru hiyo sadaka ya kuteketezwa na hiyo sadaka ya dhambi kwa ajili ya Israeli yote.

25 uAkawaweka Walawi kwenye Hekalu la Bwana wakiwa na matoazi, vinubi na zeze kama ilivyoagizwa na Daudi na Gadi mwonaji wa mfalme pamoja na nabii Nathani kwani hili lilikuwa limeamriwa na Bwana kupitia manabii wake. 26 vHivyo Walawi wakasimama tayari wakiwa na ala za uimbaji za Daudi na makuhani walikuwa na tarumbeta zao.

27 wHezekia akatoa amri ya kutoa sadaka ya kuteketezwa madhabahuni. Walipoanza kutoa sadaka, wakaanza pia kumwimbia Bwana pamoja na tarumbeta na zile ala za uimbaji za Daudi mfalme wa Israeli. 28Kusanyiko lote wakaabudu kwa kusujudu, wakati waimbaji wakiwa wanaimba na wenye tarumbeta wakipiga tarumbeta zao. Yote haya yaliendelea mpaka walipomaliza kutoa ile dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa.

29 xKutoa sadaka kulipomalizika, mfalme na kila mtu aliyekuwepo pamoja naye wakapiga magoti na kuabudu. 30 yMfalme Hezekia na maafisa wake wakawaamuru Walawi kumsifu Bwana kwa maneno ya Daudi na ya Asafu mwonaji. Hivyo wakaimba sifa kwa furaha nao wakainamisha vichwa vyao na kuabudu.

31 zKisha Hezekia akasema, “Sasa mmejiweka wakfu kwa Bwana. Njooni mlete dhabihu na sadaka za shukrani Hekaluni mwa Bwana.” Hivyo kusanyiko likaleta dhabihu na sadaka za shukrani, nao wote waliokuwa na mioyo ya hiari wakaleta sadaka za kuteketezwa.

32Idadi ya sadaka za kuteketezwa zilizoletwa na kusanyiko zilikuwa mafahali sabini, kondoo dume 100 na wana-kondoo dume 200. Wote hawa walikuwa kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa kwa Bwana. 33Wanyama waliowekwa wakfu kwa sadaka ya kuteketezwa walikuwa mafahali 600, pamoja na kondoo na mbuzi 3,000. 34 aaLakini makuhani walikuwa wachache sana kuweza kuchuna wale wanyama wote wa sadaka za kuteketezwa, kwa hiyo ndugu zao Walawi wakawasaidia mpaka kazi ile ikakamilika na mpaka makuhani wengine walipowekwa wakfu, kwa kuwa Walawi walikuwa makini kujiweka wakfu kuliko walivyokuwa makuhani. 35 abKulikuwa na sadaka nyingi za kuteketezwa, pamoja na mafuta ya wanyama ya sadaka za amani na sadaka za kinywaji ambazo ziliambatana na sadaka za kuteketezwa.

Kwa hiyo huduma ya Hekalu la Bwana ikarudishwa kwa upya.
36 acHezekia pamoja na watu wote wakafurahi kwa sababu ya lile Mungu alilolifanya kwa ajili ya watu wake, kwa kuwa lilitendeka papo hapo.

Copyright information for SwhNEN