‏ 2 Chronicles 12

Shishaki Ashambulia Yerusalemu

(1 Wafalme 14:25-28)

1 aBaada ya nafasi ya Rehoboamu kuimarika na kuwa na nguvu, yeye na Israeli yote waliiacha sheria ya Bwana Mungu. 2 bKwa sababu hawakuwa waaminifu kwa Bwana, Shishaki mfalme wa Misri akashambulia Yerusalemu katika mwaka wa tano wa utawala wa Mfalme Rehoboamu. 3 cAkiwa na magari ya vita 1,200 na wapanda farasi 60,000 na idadi isiyohesabika ya majeshi ya Walibia, Wasukii na Wakushi
Yaani watu kutoka sehemu ya Naili ya juu.
yaliyokuja pamoja naye kutoka Misri.
4 eAkateka miji ya Yuda yenye ngome akaendelea mpaka Yerusalemu.

5 fNdipo nabii Shemaya akaja kwa Rehoboamu na kwa viongozi wa Yuda waliokuwa wamekusanyika huko Yerusalemu kwa ajili ya hofu ya Shishaki naye akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana, ‘Ninyi mmeniacha mimi, kwa hiyo, mimi nami sasa ninawaacha ninyi mkononi mwa Shishaki.’ ”

6 gViongozi wa Israeli na mfalme wakajinyenyekeza na kusema, “Bwana Mungu ni mwenye haki.”

7 h Bwana Mungu alipoona kwamba wamejinyenyekeza, neno hili la Bwana likamjia Shemaya: “Maadamu wamejinyenyekeza, sitawaangamiza bali hivi karibuni nitawapatia wokovu. Ghadhabu yangu haitamwagwa juu ya Yerusalemu kwa kupitia Shishaki. 8 iHata hivyo, watamtumikia Shishaki ili wapate kujifunza tofauti kati ya kunitumikia mimi na kuwatumikia wafalme wa nchi nyingine.”

9 jShishaki mfalme wa Misri alipoishambulia Yerusalemu, alichukua hazina za Hekalu la Bwana na hazina za jumba la kifalme. Akachukua kila kitu, pamoja na zile ngao za dhahabu ambazo Solomoni alikuwa amezitengeneza. 10 kKwa hiyo Mfalme Rehoboamu akatengeneza ngao za shaba badala ya zile za dhahabu na kuzikabidhi kwa majemadari wa ulinzi wa zamu kwenye ingilio la jumba la mfalme. 11Kila wakati mfalme alipokwenda katika Hekalu la Bwana walinzi walikwenda pamoja naye wakiwa wamebeba hizo ngao na baadaye walizirudisha kwenye chumba cha ulinzi.

12 lKwa sababu Rehoboamu alijinyenyekeza, hasira ya Bwana ikageukia mbali naye, hakuangamizwa kabisa. Kukawa na hali nzuri katika Yuda.

13 mMfalme Rehoboamu akajiweka imara katika Yerusalemu na akaendelea kuwa mfalme. Alikuwa na umri wa miaka arobaini na mmoja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na saba, mji ambao Bwana alikuwa ameuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli ili aliweke Jina lake humo. Mama yake aliitwa Naama, alikuwa Mwamoni. 14 nRehoboamu akatenda maovu kwa sababu hakuuelekeza moyo wake katika kumtafuta Bwana Mungu.

15 oKwa habari ya matukio katika utawala wa Rehoboamu, tangu mwanzo mpaka mwisho, je, hayakuandikwa katika kumbukumbu za nabii Shemaya na mwonaji Ido zinazohusiana na vizazi? Kulikuwako na vita mara kwa mara kati ya Rehoboamu na Yeroboamu. 16 pRehoboamu akalala na baba zake, akazikwa katika Mji wa Daudi. Naye Abiya mwanawe akawa mfalme baada yake.

Copyright information for SwhNEN