‏ 1 Chronicles 14

Nyumba Ya Daudi Na Jamaa Yake

(2 Samweli 5:11-16)

1 aBasi Hiramu mfalme wa Tiro akawatuma wajumbe kwa Daudi, wakiwa na magogo ya mierezi, waashi na maseremala ili kumjengea jumba la kifalme. 2 bNaye Daudi akatambua kwamba Bwana amemwimarisha kuwa mfalme juu ya Israeli na kwamba ufalme wake umetukuzwa kwa ajili ya Israeli, watu wake.

3 cHuko Yerusalemu Daudi akaoa wake wengine zaidi na akawa baba wa wana na mabinti wengi. 4 dHaya ndiyo majina ya watoto waliozaliwa kwake huko: Shamua, Shobabu, Nathani, Solomoni, 5Ibihari, Elishua, Elpeleti, 6Noga, Nefegi, Yafia, 7Elishama, Beeliada na Elifeleti.

Daudi Awashinda Wafilisti

(2 Samweli 5:17-25)

8 eWafilisti waliposikia kuwa Daudi ametiwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli yote, wakapanda na jeshi lao lote kwenda kumsaka, lakini Daudi akapata habari hizo, naye akatoka ili kwenda kukabiliana nao. 9 fBasi Wafilisti walikuwa wameingia na kushambulia Bonde la Warefai, 10Hivyo Daudi akamuuliza Mungu: “Je, niende kuwashambulia hao Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?”

Bwana akamjibu, “Nenda, nitawatia mikononi mwako.”

11 gHivyo Daudi pamoja na watu wake wakakwea mpaka Baal-Perasimu,
Maana yake ni Bwana Afurikae.
akawashinda huko. Akasema, “Kama maji yafurikavyo, Mungu amewafurikia adui zangu kwa kutumia mkono wangu.” Kwa hiyo mahali pale pakaitwa Baal-Perasimu.
12 iWafilisti walikuwa wameacha miungu yao huko, Daudi akaamuru iteketezwe kwa moto.

13 jKwa mara nyingine Wafilisti wakavamia lile bonde; 14 khivyo Daudi akamuuliza Mungu tena, naye Mungu akamjibu, “Usiwapandie moja kwa moja, bali wazungukie na uwashambulie kutoka mbele ya hiyo miti ya miforosadi. 15Mara usikiapo sauti ya kwenda juu ya hiyo miti ya miforosadi, hapo ndipo utoke upigane vita, kwa sababu hiyo itaonyesha kwamba Mungu amekutangulia ili kupiga jeshi la Wafilisti.” 16 lKwa hiyo Daudi akafanya kama alivyoagizwa na Mungu, wakalipiga jeshi la Wafilisti kuanzia Gibeoni hadi Gezeri.

17 mHivyo umaarufu wa Daudi ukaenea katika kila nchi, naye Bwana akayafanya mataifa yote kumwogopa Daudi.

Copyright information for SwhNEN