‏ Psalms 58

Mungu Kuwaadhibu Waovu

Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu!” Utenzi wa Daudi.

1Enyi watawala, je, kweli mwanena kwa haki?
Je, mnahukumu kwa unyofu miongoni mwa watu?
2 aLa, mioyoni mwenu mnatunga udhalimu,
na mikono yenu hupima jeuri duniani.
3 bWaovu ni wapotovu tangu kuzaliwa kwao,
toka tumboni mwa mama zao
ni wakaidi na husema uongo.
4 cSumu yao ni kama sumu ya nyoka,
kama ile ya fira ambaye ameziba masikio yake,
5 dambaye hatasikia sauti ya kutumbuiza ya mwaguzi,
hata kama mganga angecheza kwa ustadi kiasi gani.

6 eEe Mungu, yavunje meno katika vinywa vyao;
Ee Bwana, vunja meno makali ya hao simba!
7 fNa watoweke kama maji yapitayo kwa kasi,
wavutapo pinde zao, mishale yao na iwe butu.
8 gKama konokono ayeyukavyo akitembea,
kama mtoto aliyezaliwa akiwa mfu,
wasilione jua.
9 hKabla vyungu vyenu havijapata moto wa kuni za miiba,
zikiwa mbichi au kavu,
waovu watakuwa
wamefagiliwa mbali.
10 iWenye haki watafurahi waonapo wakilipizwa kisasi,
watakapochovya nyayo zao katika damu ya waovu.
11 jNdipo wanadamu watasema,
“Hakika utulivu wa wenye haki bado una thawabu,
hakika kuna Mungu ahukumuye dunia.”
Copyright information for SwhNEN