‏ Numbers 10

Tarumbeta Za Fedha

1 Bwana akamwambia Mose: 2 a“Tengeneza tarumbeta mbili za fedha ya kufua, uzitumie kwa kuita jumuiya pamoja na wakati wa kuvunja makambi ili kuondoka. 3Tarumbeta zote mbili zikipigwa, jumuiya yote itakusanyika mbele yako katika ingilio la Hema la Kukutania. 4 bKama tarumbeta moja tu ikipigwa, viongozi, yaani wakuu wa koo za Israeli, ndio watakaokusanyika mbele yako. 5Wakati mlio wa kujulisha hatari ukipigwa, makabila yaliyo na makambi upande wa mashariki yataondoka. 6Ukisikika mlio wa pili wa jinsi hiyo, walioko kwenye makambi ya kusini wataondoka. Mlio huo wa kujulisha hatari utakuwa ishara ya kuondoka. 7 cIli kukusanya kusanyiko, piga tarumbeta zote, lakini siyo kwa mlio wa kujulisha hatari.

8 d“Wana wa Aroni, makuhani, ndio watakaopiga hizo tarumbeta. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa ajili yenu na kwa vizazi vijavyo. 9 eWakati mtakapopigana vita katika nchi yenu wenyewe dhidi ya adui anayewaonea, piga tarumbeta kwa mlio wa kujulisha hatari. Ndipo utakumbukwa na Bwana Mungu wenu na kuokolewa kutoka kwa adui zenu. 10 fPia nyakati za furaha yenu, yaani sikukuu zenu zilizoamriwa na sikukuu za Mwezi Mwandamo, mtapiga tarumbeta juu ya sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za amani, nazo zitakuwa ukumbusho kwa ajili yenu mbele za Mungu wenu. Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.”

Waisraeli Waondoka Sinai

11 gKatika siku ya ishirini ya mwezi wa pili wa mwaka wa pili, wingu liliinuka kutoka juu ya maskani ya Ushuhuda. 12 hNdipo Waisraeli wakaondoka kutoka Jangwa la Sinai wakasafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine mpaka wingu lilipotua katika Jangwa la Parani. 13 iWaliondoka kwa mara ya kwanza kwa agizo la Bwana kupitia kwa Mose.

14 jVikosi vya kambi ya Yuda vilitangulia kwanza chini ya alama yao. Nashoni mwana wa Aminadabu alikuwa kiongozi wao. 15 kNethaneli mwana wa Suari alikuwa kiongozi wa kabila la Isakari, 16 lnaye Eliabu mwana wa Heloni alikuwa kiongozi wa kabila la Zabuloni. 17 mNdipo Maskani iliposhushwa, nao wana wa Gershoni na wana wa Merari ambao waliibeba wakaondoka.

18 nVikosi vya kambi ya Reubeni vilifuata, chini ya alama yao. Elisuri mwana wa Shedeuri alikuwa kiongozi wao. 19Shelumieli mwana wa Surishadai aliongoza kikosi cha kabila la Simeoni, 20 onaye Eliasafu mwana wa Deueli aliongoza kikosi cha kabila la Gadi. 21 pKisha Wakohathi wakaondoka, wakichukua vitu vitakatifu. Maskani ilikuwa isimamishwe kabla wao hawajafika.

22 qVikosi vya kambi ya Efraimu vilifuata, chini ya alama yao. Elishama mwana wa Amihudi alikuwa kiongozi wao. 23Gamalieli mwana wa Pedasuri aliongoza kikosi cha kabila la Manase, 24 rnaye Abidani mwana wa Gideoni alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Benyamini.

25 sMwishowe, kama kikosi cha nyuma cha ulinzi wa vikosi vyote, vikosi vya kambi ya Dani viliondoka chini ya alama yao. Ahiezeri mwana wa Amishadai alikuwa kiongozi wao. 26Pagieli mwana wa Okrani aliongoza kikosi cha kabila la Asheri, 27naye Ahira mwana wa Enani aliongoza kikosi cha kabila la Naftali. 28 tHuu ndio ulikuwa utaratibu wa kuondoka wa vikosi vya Waisraeli walipokuwa wanaondoka.

29 uBasi Mose akamwambia Hobabu mwana wa Reueli, Mmidiani, mkwewe Mose, “Tunaondoka kwenda mahali ambapo Bwana amesema ‘Nitawapa ninyi mahali hapo.’ Twende pamoja nasi tutakutendea mema, kwa maana Bwana ameahidi mambo mema kwa Israeli.”

30 vAkajibu, “Hapana, sitakwenda; nitarudi kwenye nchi yangu mwenyewe na watu wangu mwenyewe.”

31 wLakini Mose akasema, “Tafadhali usituache. Wewe unajua mahali ambapo yatupasa kupiga kambi jangwani, nawe unaweza kuwa macho yetu. 32 xIkiwa utafuatana nasi, tutashirikiana nawe mema yoyote tutakayopewa na Bwana.”

33 yHivyo waliondoka kutoka mlima wa Bwana, nao wakasafiri kwa siku tatu. Sanduku la Agano la Bwana liliwatangulia kwa zile siku tatu ili kuwatafutia mahali pa kupumzika. 34 zWingu la Bwana lilikuwa juu yao wakati wa mchana walipoondoka kambini.

35 aaWakati wowote Sanduku lilipoondoka, Mose alisema,

“Ee Bwana, inuka!
Watesi wako na watawanyike;
adui zako na wakimbie mbele zako.”
36 abWakati wowote Sanduku liliposimama, alisema,

“Ee Bwana, rudi,
kwa maelfu ya Waisraeli wasiohesabika.”
Copyright information for SwhNEN