‏ Nehemiah 13

Nehemia Afanya Matengenezo Ya Mwisho

1 aSiku hiyo, Kitabu cha Mose kilisomwa kwa sauti kuu, na watu wote wakasikia. Humo ilionekana imeandikwa kwamba hakuna Mwamoni wala Mmoabu atakayeruhusiwa katika kusanyiko la watu wa Mungu, 2 bkwa sababu hawakuwalaki Waisraeli kwa chakula na maji. Badala yake walimwajiri Balaamu kuwalaani (lakini hata hivyo Mungu wetu aligeuza laana kuwa baraka). 3 cWatu waliposikia sheria hii, waliwatenga watu wote wasio Waisraeli waliokuwa wa uzao wa kigeni.

4 dKabla ya hili, kuhani Eliashibu alikuwa amewekwa kuwa msimamizi wa vyumba vya ghala ya nyumba ya Mungu wetu. Alikuwa na uhusiano wa karibu na Tobia, 5 enaye alikuwa amempa Tobia chumba kikubwa ambacho mwanzo kilikuwa kikitumika kuweka sadaka za nafaka, uvumba na vyombo vya Hekalu, pamoja na zaka za nafaka, divai mpya na mafuta waliyoagizwa Waisraeli kwa ajili ya Walawi, waimbaji na mabawabu wa lango, pamoja na matoleo kwa makuhani.

6 fLakini wakati haya yote yalipokuwa yakitendeka, sikuwa Yerusalemu, kwa kuwa katika mwaka wa thelathini na mbili wa utawala wa Artashasta mfalme wa Babeli nilikuwa nimerudi kwa mfalme. Baadaye nilimwomba ruhusa, 7 gnikarudi Yerusalemu. Hapo niligundua jambo la uovu alilofanya Eliashibu kwa kumpa Tobia chumba katika nyua za nyumba ya Mungu. 8 hNilikasirika sana na nikavitupa nje vyombo vyote vya Tobia. 9 iNilitoa amri kutakasa vyumba, kisha nikavirudisha vifaa vya nyumba ya Mungu, pamoja na sadaka za nafaka na uvumba.

10 jPia niligundua kuwa mafungu yaliyopangwa kupewa Walawi hawakuwa wamepewa, nao Walawi wote na waimbaji waliowajibika kwa huduma walikuwa wamerudi katika mashamba yao. 11 kBasi niliwakemea maafisa na kuwauliza, “Kwa nini nyumba ya Mungu imepuuzwa?” Kisha niliwaita pamoja na kuwaweka kwenye nafasi zao.

12 lYuda wote walileta zaka za nafaka, divai mpya na mafuta kwenye ghala. 13 mNikamweka kuhani Shelemia, mwandishi Sadoki, na Mlawi aliyeitwa Pedaya kuwa wasimamizi wa ghala, na kumfanya Hanani mwana wa Zakuri, mwana wa Matania kuwa msaidizi wao, kwa sababu watu hawa walionekana kuwa waaminifu. Walipewa wajibu wa kugawa mahitaji kwa ndugu zao.

14 nEe Mungu wangu, unikumbuke kwa hili, wala usifute kile nilichokifanya kwa uaminifu kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu na kwa ajili ya huduma yake.

15 oSiku hizo nikaona watu katika Yuda wakikanyaga mashinikizo ya divai siku ya Sabato na kuleta nafaka wakiwapakiza punda, pamoja na divai, zabibu, tini na aina nyingine za mizigo. Nao walikuwa wakileta haya yote Yerusalemu siku ya Sabato. Kwa hiyo niliwaonya dhidi ya kuuza vyakula siku hiyo. 16 pWatu kutoka Tiro waliokuwa wakiishi Yerusalemu walileta samaki na aina nyingi za bidhaa na kuziuza Yerusalemu siku ya Sabato kwa watu wa Yuda. 17 qNiliwakemea wakuu wa Yuda na kuwaambia, “Ni uovu gani huu mnaofanya wa kuinajisi siku ya Sabato? 18 rJe, baba zenu hawakufanya mambo kama haya, hata wakamsababisha Mungu wetu kuleta maafa haya yote juu yetu na juu ya mji huu? Sasa bado mnazidi kuchochea ghadhabu yake dhidi ya Israeli kwa kuinajisi Sabato.”

19 sWakati vivuli vya jioni vilipoangukia juu ya malango ya Yerusalemu kabla ya Sabato, niliamuru milango ifungwe, wala isifunguliwe mpaka Sabato iishe. Nikawaweka baadhi ya watu wangu mwenyewe kwenye malango ili pasiwepo mzigo utakaoingizwa ndani siku ya Sabato. 20Mara moja au mbili wachuuzi na wauzaji wa bidhaa za aina zote walilala usiku nje ya mji wa Yerusalemu. 21Lakini niliwaonya na kuwaambia, “Kwa nini mnalala karibu na ukuta? Kama mkifanya hivi tena, nitawaadhibu.” Kuanzia wakati ule hawakuja tena siku ya Sabato. 22 tKisha nikawaamuru Walawi kujitakasa na kwenda kulinda malango ili kutunza Sabato iwe takatifu.

Ee Mungu wangu, unikumbuke kwa ajili ya hili pia, nawe unionyeshe wema wako sawasawa na upendo wako mkuu.

23 uZaidi ya hayo, niliona Wayahudi waliokuwa wameoa wanawake kutoka Ashdodi, Amoni na Moabu. 24 vNusu ya watoto wao walizungumza lugha ya Kiashidodi au lugha ya watu wengine, bali hawakuweza kuzungumza Kiyahudi. 25 wNiliwakemea na kuwalaani. Niliwapiga baadhi ya watu na kungʼoa nywele zao. Niliwaapisha kwa jina la Mungu na kusema: “Msiwaoze binti zenu kwa wana wao, wala binti zao wasiolewe na wana wenu wala ninyi wenyewe. 26 xJe, Solomoni hakutenda dhambi kwa sababu ya wanawake wa namna hiyo? Miongoni mwa mataifa mengi hapakuwepo mfalme kama yeye. Alipendwa na Mungu wake. Naye Mungu alimweka kuwa mfalme juu ya Israeli yote, lakini hata yeye, wanawake wa mataifa mengine walimfanya atende dhambi. 27 yJe, tulazimike sasa kusikia kwamba ninyi pia mmefanya uovu huu mkubwa na kutokuwa waaminifu kwa Mungu wetu kwa kuoa wanawake wa kigeni?”

28 zMmoja wa wana wa Yoyada mwana wa Eliashibu kuhani mkuu alikuwa mkwewe Sanbalati Mhoroni. Nami nilimfukuza mbele yangu.

29 aaEe Mungu wangu, uwakumbuke, kwa sababu wamenajisi ukuhani, na agano la kikuhani na la Walawi.

30 abKwa hiyo niliwatakasa makuhani na Walawi kutokana na chochote kilichokuwa cha kigeni, na kuwapa wajibu, kila mmoja katika kazi yake. 31 acPia nilihakikisha kwamba matoleo ya kuni yaliletwa kwa wakati unaopaswa, na malimbuko kwa wakati wake.

Ee Mungu wangu, unikumbuke, unitendee mema.

Copyright information for SwhNEN