‏ Nahum 2

Ninawi Kuanguka

1 aMshambuliaji anasogea dhidi yako, Ninawi.
Linda ngome,
chunga barabara,
jitieni nguvu wenyewe,
kusanya nguvu zako zote!
2 b Bwana atarudisha fahari ya Yakobo,
kama fahari ya Israeli,
ingawa waangamizi wamewaacha ukiwa
na wameharibu mizabibu yao.

3 cNgao za askari wake ni nyekundu,
mashujaa wamevaa nguo nyekundu.
Chuma kwenye magari ya vita chametameta,
katika siku aliyoyaweka tayari,
mikuki ya mierezi inametameta.
4 dMagari ya vita yanafanya msukosuko barabarani,
yakikimbia nyuma na mbele uwanjani.
Yanaonekana kama mienge ya moto;
yanakwenda kasi kama umeme.

5 eAnaita vikosi vilivyochaguliwa,
lakini bado wanajikwaa njiani.
Wanakimbilia haraka kwenye ukuta wa mji,
ile ngao ya kuwakinga imetayarishwa.
6 fMalango ya mto yamefunguliwa wazi,
na jumba la kifalme limeanguka.
7 gImeagizwa kwamba mji uchukuliwe
na upelekwe uhamishoni.
Vijakazi wake wanaomboleza kama hua
na kupigapiga vifua vyao.
8Ninawi ni kama dimbwi,
nayo maji yake yanakauka.
Wanalia, “Simama! Simama!”
Lakini hakuna anayegeuka nyuma.
9Chukueni nyara za fedha!
Chukueni nyara za dhahabu!
Wingi wake hauna mwisho,
utajiri kutoka hazina zake zote!
10 hAmeharibiwa, ametekwa nyara, ameachwa uchi!
Mioyo inayeyuka, magoti yanalegea,
miili inatetemeka,
na kila uso umebadilika rangi.

11 iLiko wapi sasa pango la simba,
mahali ambapo waliwalisha watoto wao,
ambapo simba dume na simba jike walikwenda
na ambapo wana simba walikwenda
bila kuogopa chochote?
12 jSimba aliua mawindo ya kutosha watoto wake,
alinyonga mawindo kwa ajili ya mwenzi wake,
akijaza makao yake kwa alivyoua
na mapango yake kwa mawindo.

13 k Bwana Mwenye Nguvu Zote anatangaza,
“Mimi ni kinyume na ninyi.
Magari yenu ya vita nitayateketeza kwa moto,
na upanga utakula wana simba wako.
Sitawaachia mawindo juu ya nchi.
Sauti za wajumbe wako
hazitasikika tena.”
Copyright information for SwhNEN