‏ Matthew 19

Yesu Afundisha Kuhusu Talaka

(Marko 10:1-12)

1 aYesu alipomaliza kusema maneno haya, aliondoka Galilaya, akaenda sehemu za Uyahudi, ngʼambo ya Mto Yordani. 2 bUmati mkubwa wa watu ukamfuata, naye akawaponya huko.

3 cBaadhi ya Mafarisayo wakamjia ili kumjaribu, wakamuuliza, “Ni halali mtu kumwacha mke wake kwa sababu yoyote?”

4 dAkawajibu, “Je, hamkusoma kwamba hapo mwanzo Muumba aliwaumba mwanaume na mwanamke, 5 enaye akasema, ‘Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja’? 6 fHivyo si wawili tena, bali mwili mmoja. Kwa hiyo alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”

7 gWakamuuliza, “Kwa nini basi Mose aliagiza mtu kumpa mkewe hati ya talaka na kumwacha?”

8Yesu akawajibu, “Mose aliwaruhusu kuwaacha wake zenu kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Lakini tangu mwanzo haikuwa hivyo. 9 hMimi nawaambia, yeyote amwachaye mkewe isipokuwa kwa sababu ya uasherati naye akaoa mke mwingine, anazini. Naye amwoaye yule mwanamke aliyeachwa pia anazini.”

10 iWanafunzi wake wakamwambia, “Kama hali ndiyo hii kati ya mume na mke, ni afadhali mtu asioe!”

11 jYesu akawaambia, “Si watu wote wanaoweza kupokea neno hili, isipokuwa wale tu waliojaliwa na Mungu. 12 kKwa maana wengine ni matowashi kwa sababu wamezaliwa hivyo; wengine wamefanywa matowashi na wanadamu; na wengine wamejifanya matowashi kwa ajili ya Ufalme wa Mbinguni. Yeye awezaye kulipokea neno hili na alipokee.”

Yesu Awabariki Watoto Wadogo

(Marko 10:13-16; Luka 18:15-17)

13 lKisha watoto wadogo wakaletwa kwa Yesu ili aweke mikono yake juu yao na awaombee. Lakini wanafunzi wake wakawakemea wale waliowaleta.

14 mYesu akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mbinguni ni wa wale walio kama hawa.” 15Naye akaweka mikono yake juu yao, na akaondoka huko.

Kijana Tajiri

(Marko 10:17-31; Luka 18:18-30)

16 nMtu mmoja akamjia Yesu na kumuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye jambo gani jema ili nipate uzima wa milele?”

17 oYesu akamjibu, “Mbona unaniuliza habari ya mema? Aliye mwema ni Mmoja tu. Lakini ukitaka kuingia uzimani, zitii amri.”

18 pYule mtu akamuuliza, “Amri zipi?”

Yesu akamjibu, “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo,
19 qwaheshimu baba yako na mama yako, na umpende jirani yako kama nafsi yako.”

20Yule kijana akasema, “Hizi zote nimezishika. Je, bado nimepungukiwa na nini?”

21 rYesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo, na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”

22 sYule kijana aliposikia hayo, akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

Hatari Za Utajiri

23 tNdipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Amin, nawaambia, itakuwa vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mbinguni. 24Tena nawaambia, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”

25Wanafunzi wake waliposikia haya, walishangaa sana na kuuliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”

26 uLakini Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini mambo yote yanawezekana kwa Mungu.”

27 vNdipo Petro akamjibu, “Tazama, sisi tumeacha kila kitu na kukufuata! Tutapata nini basi?”

28 wYesu akawaambia, “Amin, nawaambia, wakati wa kufanywa upya vitu vyote, Mwana wa Adamu atakapoketi kwenye kiti chake kitukufu cha enzi, ninyi mlionifuata pia mtaketi katika viti vya enzi kumi na viwili, mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. 29 xKila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu zake wa kiume au wa kike, baba au mama, watoto au mashamba kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi ya hayo, na ataurithi uzima wa milele. 30 yLakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.

Copyright information for SwhNEN