‏ Jeremiah 19

Gudulia La Udongo Lililovunjika

1 aHili ndilo asemalo Bwana: “Nenda ukanunue gudulia la udongo kutoka kwa mfinyanzi. Wachukue baadhi ya wazee wa watu na wa makuhani 2 bna mtoke mwende mpaka kwenye Bonde la Ben-Hinomu, karibu na ingilio la Lango la Vigae. Huko tangaza maneno ninayokuambia, 3 cnawe useme, ‘Sikieni neno la Bwana, enyi wafalme wa Yuda na watu wa Yerusalemu. Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: Sikilizeni! Nitaleta maafa mahali hapa, ambayo yatafanya masikio ya kila mmoja atakayesikia habari zake yawashe. 4 dKwa kuwa wameniacha na kupafanya mahali hapa kuwa pa miungu ya kigeni. Wameiteketezea sadaka miungu ambayo wao wala baba zao wala wafalme wa Yuda kamwe hawakuijua, nao wamelijaza eneo hili kwa damu isiyo na hatia. 5 eWamejenga mahali pa juu pa kuabudia miungu pa Baali ili kuteketeza wana wao katika moto kama sadaka kwa Baali, kitu ambacho sikukiamuru wala kukitaja, wala hakikuingia akilini mwangu. 6 fHivyo jihadharini, siku zinakuja, asema Bwana, wakati watu hawatapaita tena mahali hapa Tofethi ama Bonde la Ben-Hinomu, bali Bonde la Machinjo.

7 g“ ‘Nitaiharibu mipango ya Yuda na Yerusalemu mahali hapa. Nitawafanya waanguke kwa upanga mbele ya adui zao, katika mikono ya wale watafutao uhai wao, nami nitaitoa mizoga yao kuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi. 8 hNitauharibu mji huu na kuufanya kitu cha kudharauliwa. Wote wapitao karibu watashangaa na kuudhihaki kwa sababu ya majeraha yake yote. 9 iNitawafanya wao kula nyama ya wana wao na binti zao; kila mmoja atakula nyama ya mwenzake wakati wa dhiki ya kuzungukwa na jeshi lililowekwa juu yao na adui wanaotafuta uhai wao.’

10 j“Kisha livunje lile gudulia wale walio pamoja nawe wakiwa wanaangalia, 11 kuwaambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo: Nitalivunja taifa hili na mji huu kama gudulia hili la mfinyanzi lilivyovunjwa, nalo haliwezi kutengenezeka tena. Watawazika waliokufa huko Tofethi hata isiwepo nafasi zaidi. 12Hivi ndivyo nitakavyopafanya mahali hapa na kwa wale waishio ndani yake, asema Bwana. Nitaufanya mji huu kama Tofethi. 13 lNyumba zilizoko Yerusalemu na zile za wafalme wa Yuda zitatiwa unajisi kama mahali hapa, Tofethi: yaani nyumba zote ambazo walifukiza uvumba juu ya mapaa yake kwa jeshi lote la angani, na kumimina dhabihu za vinywaji kwa miungu mingine.’ ”

14 mKisha Yeremia akarudi kutoka Tofethi, mahali ambapo Bwana alikuwa amemtuma kutoa unabii, akasimama katika ua wa Hekalu la Bwana na kuwaambia watu wote, 15 n“Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Sikilizeni! Nitaleta juu ya mji huu pamoja na vijiji vinavyouzunguka kila maafa niliyosema dhidi yake, kwa sababu wamekuwa na shingo ngumu, na hawakuyasikiliza maneno yangu.’ ”

Copyright information for SwhNEN