‏ Jeremiah 13

Mkanda Wa Kitani

1Hili ndilo Bwana aliloniambia: “Nenda ununue mkanda wa kitani, ujivike kiunoni mwako, lakini usiuache uguse maji.” 2Kwa hiyo nikanunua mkanda, kama Bwana alivyoniagiza, nikajivika kiunoni.

3 aNdipo neno la Bwana likanijia kwa mara ya pili: 4 b“Chukua mkanda ulionunua ambao umeuvaa kiunoni mwako, uende sasa Frati uufiche ndani ya ufa mdogo kwenye mwamba.” 5 cNdipo nikaenda na kuuficha ule mkanda huko Frati, kama Bwana alivyoniamuru.

6Baada ya siku nyingi Bwana akaniambia, “Nenda sasa Frati ukauchukue ule mkanda niliokuambia uufiche huko.” 7 dHivyo nikaenda Frati na kuuchimbua ule mkanda kutoka pale nilipokuwa nimeuficha, lakini sasa ulikuwa umeharibika na haufai tena kabisa.

8Ndipo neno la Bwana likanijia: 9 e“Hili ndilo Bwana asemalo: ‘Vivyo hivyo ndivyo nitakavyokiharibu kiburi cha Yuda na kiburi kikuu cha Yerusalemu. 10 fWatu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wafuatao ukaidi wa mioyo yao na kufuata miungu mingine kuitumikia na kuiabudu, watakuwa kama mkanda huu ambao haufai kabisa! 11 gKwa maana kama vile mkanda ufungwavyo kiunoni mwa mtu, ndivyo nilivyojifunga nyumba yote ya Israeli na nyumba yote ya Yuda,’ asema Bwana, ‘ili wawe watu wangu kwa ajili ya utukufu wangu, sifa na heshima yangu. Lakini hawajasikiliza.’

Viriba Vya Mvinyo

12“Waambie: ‘Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, asemalo: kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo.’ Kama wao wakikuambia, ‘Kwani hatujui kwamba kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo?’ 13 hKisha uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: nitawajaza ulevi wote waishio katika nchi hii, pamoja na wafalme waketio juu ya kiti cha enzi cha Daudi, makuhani, manabii na wale wote waishio Yerusalemu. 14 iNitawagonganisha kila mmoja na mwenzake, baba na wana wao, asema Bwana. Sitawarehemu wala kuwahurumia ili niache kuwaangamiza.’ ”

Tishio La Kutekwa

15Sikieni na mzingatie,
msiwe na kiburi,
kwa kuwa Bwana amenena.
16 jMpeni utukufu Bwana Mungu wenu,
kabla hajaleta giza,
kabla miguu yenu haijajikwaa
juu ya vilima vitakavyotiwa giza.
Mlitarajia nuru,
lakini ataifanya kuwa giza nene
na kuibadili kuwa huzuni kubwa.
17 kLakini kama hamtasikiliza,
nitalia sirini
kwa ajili ya kiburi chenu;
macho yangu yatalia kwa uchungu,
yakitiririka machozi,
kwa sababu kundi la kondoo la Bwana
litachukuliwa mateka.

18 lMwambie mfalme na mamaye,
“Shukeni kutoka kwenye viti vyenu vya enzi,
kwa kuwa taji zenu za utukufu
zitaanguka kutoka vichwani mwenu.”
19 mMiji iliyoko Negebu itafungwa,
wala hapatakuwa na mtu wa kuifungua.
Watu wa Yuda wote watapelekwa uhamishoni,
wakichukuliwa kabisa waende mbali.

20 nInua macho yako uone
wale wanaokuja kutoka kaskazini.
Liko wapi lile kundi ulilokabidhiwa,
kondoo wale uliojivunia?
21 oUtasema nini Bwana atakapowaweka juu yako
wale ulioungana nao kama marafiki wako maalum?
Je, hutapatwa na utungu kama mwanamke
aliye katika utungu wa kuzaa?
22 pNawe kama ukijiuliza,
“Kwa nini haya yamenitokea?”
Ni kwa sababu ya dhambi zako nyingi
ndipo marinda yako yameraruliwa
na mwili wako umetendewa vibaya.
23Je, Mkushi aweza kubadili ngozi yake
au chui kubadili madoadoa yake?
Vivyo hivyo nawe huwezi kufanya mema
wewe uliyezoea kutenda mabaya.

24 q“Nitawatawanya kama makapi
yapeperushwayo na upepo wa jangwani.
25 rHii ndiyo kura yako,
fungu nililokuamuria,”
asema Bwana,
“kwa sababu umenisahau mimi
na kuamini miungu ya uongo.
26 sNitayafunua marinda yako mpaka juu ya uso wako
ili aibu yako ionekane:
27 tuzinzi wako na kulia kwako kama farasi kulikojaa tamaa,
ukahaba wako usio na aibu!
Nimeyaona matendo yako ya machukizo
juu ya vilima na mashambani.
Ole wako, ee Yerusalemu!
Utaendelea kuwa najisi mpaka lini?”
Copyright information for SwhNEN