‏ Genesis 24

Isaki Na Rebeka

1 aWakati huu Abrahamu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, naye Bwana alikuwa amembariki katika kila njia. 2 bAkamwambia mtumishi wake mkuu wa vitu vyote katika nyumba yake, yule aliyekuwa msimamizi wa vitu vyote alivyokuwa navyo, “Weka mkono wako chini ya paja langu, 3 cNinataka uape kwa Bwana, Mungu wa mbingu na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke kutoka binti za Wakanaani, ambao ninaishi miongoni mwao, 4 dbali utakwenda katika nchi yangu na jamaa zangu umpatie Isaki mwanangu mke.”

5 eYule mtumishi akamuuliza, “Je, kama huyo mwanamke atakataa kuja nami katika nchi hii? Je, nimpeleke mwanao katika hiyo nchi uliyotoka?”

6Abrahamu akasema, “Hakikisha kwamba hutamrudisha mwanangu huko. 7 fBwana, Mungu wa mbingu, aliyenitoa nyumbani kwa baba yangu na nchi yangu niliyozaliwa na aliyesema nami na akaniahidi kwa kiapo, akisema, ‘Nitawapa watoto wako nchi hii,’ atatuma malaika wake akutangulie ili umpatie mwanangu mke kutoka huko. 8 gKama huyo mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi utafunguliwa kutoka kiapo nilichokuapisha. Ila usimrudishe mwanangu huko.” 9 hBasi yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la bwana wake Abrahamu akamwapia kuhusu shauri hili.

10 iNdipo huyo mtumishi akachukua ngamia kumi miongoni mwa ngamia za bwana wake, akaondoka, akiwa amechukua aina zote za vitu vizuri kutoka kwa bwana wake. Akaelekea Aramu-Naharaimu
Yaani Mesopotamia ya Kaskazini-Magharibi.
na kushika njia kwenda mji wa Nahori.
11 kAkawapigisha ngamia magoti karibu na kisima cha maji nje ya mji, ilikuwa inaelekea jioni, wakati ambapo wanawake wanakuja kuteka maji.

12 lKisha akaomba, “Ee Bwana, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, nipatie ushindi leo, uonyeshe huruma kwa bwana wangu Abrahamu. 13Tazama, nimesimama karibu na kisima hiki cha maji, nao binti za watu wa mji huu wanakuja kuteka maji. 14 mBasi na iwe hivi, nitakapomwambia binti mmojawapo, ‘Tafadhali tua mtungi wako nipate kunywa maji,’ naye akisema, ‘Kunywa, nitawanywesha na ngamia wako pia.’ Basi na awe ndiye uliyemchagua kwa ajili ya mtumishi wako Isaki. Kwa hili nitajua umemhurumia bwana wangu.”

15 nIkawa kabla hajamaliza kuomba, Rebeka akatokea akiwa na mtungi begani mwake. Alikuwa binti wa Bethueli. Bethueli alikuwa mwana wa Milka aliyekuwa mke wa Nahori ndugu wa Abrahamu. 16 oHuyu msichana alikuwa mzuri sana wa sura, bikira, ambaye hakuna mtu aliyekuwa amekutana naye kimwili. Aliteremka kisimani, akajaza mtungi wake akapanda juu.

17 pNdipo yule mtumishi akaharakisha kukutana naye akamwambia, “Tafadhali nipe maji kidogo katika mtungi wako.”

18Yule msichana akasema, “Kunywa, bwana wangu.” Akashusha kwa haraka mtungi mkononi mwake na akampa, akanywa.

19Baada ya kumpa yule mtumishi yale maji, akamwambia, “Nitateka maji kwa ajili ya ngamia zako pia mpaka wote watosheke.” 20Akafanya haraka kumimina maji kwenye birika ya kunyweshea wanyama, akakimbia kisimani kuteka maji mengine na akateka ya kuwatosha ngamia wake wote. 21Pasipo kusema neno, yule mtumishi akamtazama kwa makini aone kama Bwana ameifanikisha safari yake, au la.

22 qIkawa ngamia walipokwisha kunywa wote, yule mtumishi akampa huyo msichana pete ya puani ya dhahabu yenye uzito wa beka moja
Beka moja ya dhahabu ni sawa na gramu 5.5.
na bangili mbili za dhahabu zenye uzito wa shekeli kumi.
Shekeli 10 za dhahabu ni sawa na gramu 110.
23 tKisha akamuuliza, “Wewe ni binti wa nani? Tafadhali uniambie, je, kuna nafasi katika nyumba ya baba yako tutakapoweza kulala?”

24 uYule msichana akamjibu, “Mimi ni binti wa Bethueli, mwana wa Milka aliyemzalia Nahori.” 25 vAkaendelea kusema, “Kwetu kuna majani mengi na malisho, tena kuna nafasi kwa ajili yenu kulala.”

26 wYule mtumishi akasujudu na kumwabudu Bwana, 27 xakisema, “Atukuzwe Bwana, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ambaye hakuondoa wema na uaminifu wake kwa bwana wangu. Mimi nami, Bwana ameniongoza safarini akanifikisha nyumbani kwa jamaa za bwana wangu.”

28 yYule msichana akakimbia akawaeleza watu wa nyumbani mwa mama yake kuhusu mambo haya. 29 zRebeka alikuwa na kaka aliyeitwa Labani, huyo akaharakisha kukutana na yule mtumishi kule kisimani. 30 aaMara alipoiona ile pete puani, na bangili mikononi mwa dada yake na kusikia yale maneno Rebeka aliyoambiwa na huyo mtumishi, alimwendea huyo mtumishi, akamkuta amesimama karibu na ngamia wake pale karibu na kisima. 31 abAkamwambia, “Karibu nyumbani wewe uliyebarikiwa na Bwana, kwa nini unasimama huko nje? Mimi nimekuandalia nyumba na mahali kwa ajili ya ngamia.”

32 acHivyo yule mtumishi akaenda nyumbani, mizigo ikaondolewa juu ya ngamia. Majani na malisho yakaletwa kwa ajili ya ngamia na maji kwa ajili yake na watu wake ili kunawa miguu. 33Ndipo chakula kikaandaliwa kwa ajili yake, lakini akasema, “Sitakula mpaka niwe nimewaambia yale niliyo nayo ya kusema.”

Labani akasema, “Basi tuambie.”

34 adHivyo akasema, “Mimi ni mtumishi wa Abrahamu. 35 aeBwana amembariki sana bwana wangu, amekuwa tajiri. Amempa kondoo na ngʼombe, fedha na dhahabu, watumishi wa kiume na wa kike, ngamia na punda. 36 afSara mkewe bwana wangu amemzalia mwana katika uzee wake, naye amempa kila kitu alichokuwa nacho. 37 agNaye bwana wangu ameniapisha na akasema, ‘Kamwe usimtwalie mwanangu mke katika binti za Wakanaani, ambao ninaishi katika nchi yao, 38 ahila uende mpaka kwa jamaa ya baba yangu na ukoo wangu mwenyewe, ukamtwalie mwanangu mke huko.’

39“Kisha nikamuuliza bwana wangu, ‘Je, kama huyo mwanamke hatakubali kurudi nami?’

40 ai“Akanijibu, ‘Bwana ambaye nimetembea mbele zake, atatuma malaika wake pamoja nawe, na kuifanikisha safari yako, ili uweze kupata mke kwa ajili ya mwanangu katika ukoo wangu na kutoka jamaa ya baba yangu. 41Kisha, utakapokwenda kwenye ukoo wangu, utakuwa umefunguliwa kutoka kiapo changu hata kama wakikataa kukupa huyo binti, utakuwa umefunguliwa kutoka kiapo changu.’

42“Nilipokuja kisimani leo nilisema, ‘Ee Bwana, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ikikupendeza, naomba uifanikishe safari niliyoijia. 43 ajTazama, ninasimama kando ya kisima hiki, kama mwanamwali akija kuteka maji nami nikimwambia, tafadhali niruhusu ninywe maji kidogo kutoka kwenye mtungi wako, 44naye kama akiniambia, “Kunywa, nami nitateka maji kwa ajili ya ngamia wako pia,” basi huyo awe ndiye mke ambaye Bwana amemchagulia mwana wa bwana wangu.’

45 ak“Kabla sijamaliza kuomba moyoni mwangu, Rebeka akatokea, amebeba mtungi begani mwake. Akashuka kisimani akateka maji, nami nikamwambia, ‘Tafadhali nipe maji ninywe.’

46“Akafanya haraka kushusha mtungi wake begani na kusema, ‘Kunywa na nitawanywesha ngamia wako pia,’ basi nikanywa, akawanywesha na ngamia pia.

47 al“Nikamuuliza, ‘Wewe ni binti wa nani?’

“Akasema, ‘Mimi ni binti wa Bethueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia.’

“Ndipo nilipotia pete puani mwake na bangili mikononi mwake,
48nikasujudu na nikamwabudu Bwana. Nikamtukuza Bwana, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, aliyeniongoza katika njia sahihi ili nimtwalie mwana na bwana wangu mke katika jamaa zake. 49Ikiwa mtaonyesha wema na uaminifu kwa bwana wangu, mniambie, la sivyo, mniambie, ili niweze kujua njia ya kugeukia.”

50 amLabani na Bethueli wakajibu, “Jambo hili limetoka kwa Bwana, hatuwezi kukuambia jambo lolote baya au jema. 51Rebeka yuko hapa, mchukue na uende, awe mke wa mwana wa bwana wako, sawasawa na Bwana alivyoongoza.”

52Ikawa huyo mtumishi wa Abrahamu aliposikia waliyosema, alisujudu mpaka nchi mbele za Bwana. 53 anNdipo huyo mtumishi akatoa vitu vilivyotengenezwa kwa dhahabu na kwa fedha pamoja na mavazi, akampa Rebeka, pia akawapa zawadi za thamani kubwa nduguye na mamaye. 54 aoKisha yeye na wale watu waliokuwa pamoja naye wakala, wakanywa na kulala palepale.

Walipoamka asubuhi, yule mtumishi, akasema, “Nipeni ruhusa nirudi kwa bwana wangu.”

55 apLakini ndugu yake Rebeka pamoja na mama yake wakajibu, “Acha binti akae kwetu siku kumi au zaidi, ndipo mwondoke.”

56Lakini yule mtumishi akawaambia, “Msinicheleweshe, kwa kuwa Bwana amefanikisha safari yangu, nipeni ruhusa nirudi kwa bwana wangu.”

57Ndipo wakasema, “Acha tumwite huyo binti tumuulize, tusikie atakavyosema.” 58 aqKwa hiyo wakamwita Rebeka na kumuuliza, “Je, utakwenda na mtu huyu?”

Akasema, “Nitakwenda.”

59 arHivyo wakamwaga ndugu yao Rebeka aondoke, pamoja na mjakazi wake, mtumishi wa Abrahamu na watu wake. 60 asWakambariki Rebeka, wakamwambia,

“Ndugu yetu, uwe wewe kumi elfu,
mara elfu nyingi,
nao wazao wako wamiliki
malango ya adui zao.”
61 atRebeka na vijakazi wake wakajiandaa, wakapanda ngamia zao wakafuatana na yule mtu. Hivyo yule mtumishi akamchukua Rebeka akaondoka.

62 auBasi Isaki alikuwa ametoka Beer-Lahai-Roi, kwa kuwa alikuwa anaishi nchi ya Negebu. 63 avIsaki akatoka kwenda shambani kutafakari wakati wa jioni, alipoinua macho yake, akaona ngamia wanakuja. 64 awRebeka pia akainua macho akamwona Isaki. Akashuka kutoka kwenye ngamia wake 65 axna akamuuliza yule mtumishi, “Ni nani mtu yule aliye kule shambani anayekuja kutulaki?”

Yule mtumishi akajibu, “Huyu ndiye bwana wangu.” Hivyo Rebeka akachukua shela yake akajifunika.

66Kisha yule mtumishi akamweleza Isaki mambo yote aliyoyatenda. 67 ayNdipo Isaki akamwingiza Rebeka katika hema la Sara mama yake, Isaki akamchukua Rebeka, hivyo akawa mke wake. Isaki akampenda, akafarijika baada ya kifo cha mama yake.

Copyright information for SwhNEN